Taarifa kutoka mjini Buni Yadi katika jimbo la Yobe
Kaskazini mwa Nigeria, zinasema kuwa watu 24 wakiwemo wanajeshi 11 wameuawa
katika shambulizi dhidi ya kambi za wanajeshi.
Inaarifiwa kuwa kundi la Boko Haram ndilo linashukiwa
kufanya mashambulizi hayo.
Wakaazi wanasema washambuliaji waliwasili katika eneo hilo
kwa magari kumi ya kawaida na gari moja la kijeshi.
Waliwaambia wanakijiji kutokuwa na hofu kwani nia yao
haikuwa kuwadhuru raia bali maafisa wa usalama.
Wanajeshi 11, polisi 13 akiwemo mwanamke mmoja waliuawa.
Pia waliteketeza majengo na magari ikiwemo makazi ya
kiongozi mmoja wa kijadi na kituo kimoja cha polisi.
Taarifa zaidi bado zinajitokeza pole pole hasa kwa kuwa
mawasiliano yamekuwa magumu kutokana na miundo mbinu mibovu.
Jimbo la Yobe ni moja ya majimbo matatu ambayo serikali
imeweka sheria ya kutotoka nje usiku. Licha ya sheria hiyo mashambulizi ya mara
kwa mara yamekuwa yakishuhudiwa mengi yakifanywa na Boko Haram.