Na Fidelis Butahe, Mwananchi
Kwa ufupi
Kwa ufupi
Asema Rais wa Marekani, Barack Obama alishinda awamu ya pili kwa sababu ya
kutengeneza ajira.
Dodoma. Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa amesema
vijana 10,500 waliojitokeza hivi karibuni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
kufanya usaili wa nafasi 70 za kazi katika Idara ya Uhamiaji, ni ishara kuwa
bomu la ajira litalipuka muda wowote.
Akizungumza na waandishi wa habari jana nje ya Viwanja vya Bunge, Lowassa
alisema Serikali ni lazima ihakikishe inatengeneza ajira kwa kuwa kila mwaka
zaidi ya vijana 30,000 wanahitimu katika vyuo mbalimbali nchini.
Wasomi hao wa fani mbalimbali walijitokeza katika uwanja huo Ijumaa
iliyopita, kuanzia saa 12 asubuhi wakisubiri kufanyiwa usaili huo.
Lowassa ambaye alijiuzulu wadhifa wa Waziri Mkuu mwaka 2008, amenukuliwa
mara nyingi akiitaka Serikali kuchukua hatua kukabiliana na tatizo la ajira na
akisema ni bomu linalosubiri kulipuka.
Mbunge huyo wa Monduli kupitia CCM, aliwahi kuingia kwenye malumbano makali
na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka kuhusiana na suala la ajira kwa
vijana.
Kabaka akiwa bungeni, Machi 21, 2012 alitoa takwimu za namna Serikali
ilivyokuwa inatengeneza ajira kwa nia ya kumjibu Lowassa, ambaye alikuwa
ameeleza tatizo la ajira linavyowaathiri vijana.
Jana, Lowassa kuongezeka kwa makundi ya vijana wanaopora watu katika maeneo
mbalimbali nchini ni ishara ya ukosefu wa ajira. “Watanzania sasa tupo milioni
48 na kila mwaka vijana zaidi ya 30,000 wanahitimu vyuo vikuu na kazi hakuna,
pamoja na hilo hatuambiwi ni vijana wangapi ambao hawana kazi,” alisema
Lowassa.
Alisema lazima Serikali itengeneze ajira kwa wananchi wake, huku akimtolea
mfano Rais wa Marekani, Barack Obama kwamba alishinda awamu ya pili kwa sababu
ya kutengeneza ajira.
“Mfano mzuri ni katika uanzishwaji wa viwanda. Tunapofikiria kuanzisha
kiwanda cha pamba kwanza lazima tuangalie tutatengeneza ajira ngapi,” alisema.
Katika kuonyesha kuwa ajira sasa ni tatizo nchini, juzi jioni wakati wa
mjadala wa Bajeti Kuu, Naibu Spika Job Ndugai alisema Mtanzania mwenye nia ya
kugombea urais mwaka 2015 ili aweze kuelekewa kwa wananchi ni lazima aeleze
mikakati ya kuwasaidia vijana kupata ajira.
“Ajira ni tatizo kubwa na lazima lishughulikiwe. Kuna vijana hawaendi shule
lazima watazamwe. Kuna wanaomaliza darasa la saba, kidato cha nne, cha sita na
vyuo vikuu. Nazungumza kutoka moyoni kabisa. Hizi ni dakika za mwisho za
Serikali ya awamu ya nne, wale wanaojipanga kwa awamu ya tano kama
hawataongelea ajira basi waandike wameumia.”
Ndugai alisema vijana wasio na kazi ndiyo wapigakura wakubwa na kusisitiza
kuwa mgombea yeyote makini ni lazima afikirie suala la ajira kwa vijana.