Mtoto Erick Emmanuel (6)mkazi wa Kijiji cha Bwizanduru Kata
ya Maruku, Wilaya ya Bukoba Vijijini, akiwa na makovu na majeraha mapya
yanayodaiwa kutokana na kipigo cha viboko kutoka kwa baba yake. Picha na
Phinias Bashaya
Kwa ufupi
- Ni wa miaka sita, alifungiwa ndani kwa miezi saba na kuchapwa bakora kila siku.
Na Phinias Bashaya, Mwananchi
Bukoba. Matukio ya ukatili yameendelea kuibuka nchini
baada ya kugundulika kwa mtoto mwenye umri wa miaka sita katika Kijiji cha
Bwizanduru Kata ya Maruku Wilaya ya Bukoba Vijijini akiwa amefungiwa ndani kwa
miezi saba huku makalio yake yakiwa yamechanika kutokana na adhabu ya viboko.
Mtoto huyo aitwaye Erick Emmanuel anatembea kwa shida huku
akiwa na makovu mengi mwilini na sehemu ya makalio yake kuharibika vibaya.
Amekuwa akipewa adhabu hiyo na baba yake mzazi.
Kwa mujibu wa majirani wa mtoto huyo ambaye anaishi na mama
yake wa kambo aitwaye Fidea Emmanuel, anayedaiwa kumtesa mtoto huyo ni baba
yake mzazi aliyejulikana kwa jina la Emmanuel Justinian.
Chanzo cha mateso hayo inadaiwa kuwa mtoto huyo hujisaidia
ndani na hivyo baba yake mzazi kuamua kumfungia kwa kipindi chote cha miezi
saba bila kutoka nje huku kila siku mtoto huyo akipata adhabu kali ya viboko.
Mama wa kambo wa mtoto huyo Fidea Emmanuel aliiambia
Mwananchi kuwa mume wake alikuwa akimpa adhabu mtoto huyo mara kwa mara hasa
alipojisaidia au kukojoa ndani kwa kutumia fimbo ya mti wa m’buni.
Hata hivyo mama huyo wa kambo na Erick alisema kutokana na
hali mbaya ya mtoto huyo iliyotokana na adhabu ya viboko,amekuwa akimtibu kwa
kutumia dawa za mitishamba bila ya kufanyiwa vipimo au kupelekwa hospitalini.
Pia, mtoto huyo anaonekana kuwa na michirizi mikubwa katika
sehemu ya kifua na tumbo pamoja na makovu makubwa mwilini mwake, alama ambazo
zinahusishwa na viboko alivyokuwa akicharazwa na baba yake mzazi.
Naye, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Maiga Audax Bayon, alisema
kuwa ilikuwa ni vigumu kumuona mtoto huyo kwa kuwa kila aliyemuulizia aliambiwa
yuko ndani akijifunza kusoma na watoto wengine jambo ambalo halikuwa kweli.
Mama mzazi wa mtoto huyo Aneth Brand ambaye anaishi Kijiji
cha Bugabo wilayani humo alisema miezi saba iliyopita alimpeleka mtoto huyo kwa
baba yake na kudai hakuwa na matatizo makubwa yanayomkabili mtoto wake, lakini
sasa ana matatizo ikiwamo upungufu wa damu.
Akizungumzia tukio hilo Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha
Bwizanduru, Edward Mwemezi alisema pamoja na mtoto huyo kufanyiwa ukatili mkubwa
kwa muda mrefu alisema familia ilijitahidi kuficha taarifa hizo hata kwa
majirani.