Vurugu kubwa imezuka mkoani Kagera wilayani Muleba, ambapo mwandishi mmoja wa gazeti la Mwananchi  Shaban Nyamukama amejikuta akipokea kichapo kutoka kwa askari polisi, huku wananchi nao wakiambulia mabomu ya machozi.


Vurugu hizo zimeibuka baada ya wananchi kuvamia chumba cha kuhifadhia maiti cha afya cha Kiagara na kuanza kuvunja. Askari polisi walifika eneo la tukio wakiambatana na amkuu wa wilaya ya Muleba, Lambris Kipuyo, na kuanza kurusha mabomu ya machozi hewani kuwatawanya wananchi hao.

Mwandishi Shabani Ndyamukama amekutwa katika vurugu hizo akiendelea na jukumu lake la kupiga picha. Askari walimshika na mwandishi huyo na kuanza kumteremshia kipigo cha mbwa mwizi huku wakidai kuwa alikuwa akifanya kazi hiyo pasipo na ruhusa yao.

Kipigo hicho kilimsababishia mwandishi huyo majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili wake, kama vile sehemu ya chini ya goti la mguu wake wa kulia, pamoja na kwenye bega lake la kushoto.  Pamoja na majeraha hayo alinyang’anywa kamer yake, recorder, na simu ya mkononi.

Kitendo cha Askari polisi kumburuza Mwandishi huyo hadi kwenye gari lao na kumuweka chini ya ulinzi kiliongeza vurugu zaidi, ambapo wananchi walipanga mawe barabarani kushinikiza kuachiwa kwa mwandishi huyo.

Baada ya waandishi wa ITV, na Redio One kanda ya ziwa kumpigia kamanda George Mayunga, ambaye alikiri kutokea kwa vurugu hizo. Muandishi aliyekuwa anashikiliwa na jeshi hilo aliachiwa huru na kwenda katika kituo cha afya cha Kiagara kupata matibabu ili kuweka sawa afya yake na ilipofika majira ya saa 8 mchana aliruhusiwa na kwenda kupumzika mjini Muleba.

Wananchi wa wilaya ya Muleba walichukua jukumu hilo la kuvunja jengo la Monchwari  wakiwa na lengo la kutaka kuchukua mwili wa msichana Asera Triphone (16) aliyepoteza maisha mkoani Arusha ambako alikuwa anafanya kazi za ndani. Iliaminika kuwa binti huyo alikuwa amekatwa baadhi ya sehemu zake za mwili kwa imani za kishirikina.

 
Top