Baada ya kuripotiwa kwa habari za mwajiri kumchoma msichana wake
wa kazi kwa pasi siku chache zilizopita, kumeibuka mengine huko Mkoani Kagera, ambapo msichana
mwenye umri wa miaka 16 amefariki dunia katika mazingira ya kutatanisha na
kukutwa baadhi ya viungo vyake vya mwili vimekatwa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha habari kimesema kuwa, Binti huyo ambaye alifahamika kwa majina ya Asera Triphone (16) aliombwa kutoka kwa wazazi wake na mwajiri, Valentina Maximilian mwaka 2013 na kwenda kufanya kazi za ndani.
Chanzo cha habari kimeendelea kueleza kuwa, wazazi wa binti huyo waliendelea kupata mawasiliano na kujua maendeleo ya mtoto wao kwa kupitia simu ya mwajiri.
Juni 13 mwaka huu 2014, mama mzazi wa binti huyo alipigiwa simu na mwajiri na kumweleza kuwa binti yake alikuwa anaumwa. Baada ya masaa mawili mwajiri huyo alipiga tena simu na kusema kuwa mgonjwa alikuwa amefariki dunia.
Wananchi walichukua jukumu la kuvunja jengo la chumba cha kuhifadhia maiti cha zahanati ya Kaigara, wakiwa na mashaka kuwa mwili wa marehemu ulikuwa umekatwa baadhi ya sehemu za mwili wake kama vile sehemu za siri, miguu, mikono kwa kinachoaminika kuwa ni imani za kishirikina.
Wananchi walipofungua jeneza waliweza kumuona marehemu kuwa ni kweli alikuwa ni mtoto wa mama huyo, lakini walipatwa na mshituko walipoukuta mwili huo umevalishwa soksi miguuni na mikononi.
Baada ya kuvuliwa soksi hizo walikuta majeraha yaliyosababishwa na kuunguzwa kwa moto mikononi na miguuni huku kichwa kikiwa na majeraha ya kukatwa na kitu chenye ncha kali.
Baada ya kuuchunguza zaidi mwili huwo uligundulika kuwa na tundu maeneo ya kwenye moyo ambalo lilikuwa limefunikwa kwa pamba, vilevile marehemu alikuwa ameng'olewa meno manne ya juu, lakini sehemu zake za siri zilikuwepo.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya ya Muleba, Lambris amekanusha taarifa hizo na kueleza kuwa, mtoto huyo alikuwa na matatizo ya kifafa wakati alipokuwa akichukuliwa na mwajiri wake, na hata wazazi wake walikuwa wanalitambua hilo. Mkuu wa wilaya amewatahadharisha wananchi kuwa makini na taarifa za uwongo zilizojaa uchochezi.
______________________________________________________________________________________