Kwa ufupi
Kuna wanandoa wamekuwa wanaishi isivyo sawa, kwamba wanaishi bila kuelewana
vizuri.
Kama unaingia kwenye ndoa kwa sababu ya kumkera fulani, fahamu kwamba hilo
ni kosa na linasababisha wakati fulani watu kujuta kwanini amekutana na fulani.
Ingawa watu wanaweza kusema kwa kadri wanavyoweza, ukweli ni kwamba utulivu
kwenye ndoa kwa asilimia kubwa huletwa na mwanamke. Utulivu huzaa mapenzi na
huruma baina ya wanandoa, kwa maana nyingine, mwanamke ana nafasi kubwa ya
kujenga au kubomoa ndoa, hii haina maana yake ni kwamba mwanamume hana nafasi
ya uharibifu, bali nafasi ya mwanzo inachukuliwa na mwanamke bila ya upinzani.
Sababu kubwa ya wanandoa kuchokana, au kuzeeka kwa ndoa kunasababishwa na
mwanamke, pale ambapo atashindwa kutumia nafasi yake na vipawa alivyopewa
kuleta utulivu katika ndoa yao, na hapa nitajaribu kujadili baadhi ya
visababishi vinavyopelekea kuzeeka kwa ndoa au kuchokana. Visababishi ambavyo
huwa vinadharaulika na kuonekana vitu vidogo vidogo hususan kwa wanawake wengi.
Wapo ambao wanaweza kukanusha hili, lakini unapaswa kujiuliza inakuwaje kama
kweli mwanaume anashiba, kwanini aende kusaka wanawake wengine kwa ajili ya
kufanya nao ngono. Huenda akawa na sababu nyingine, hata hivyo kwa asilimia
kubwa hiyo humaanisha kwamba huenda ndani ya ndoa yake kuna shida, hasa ya
kupata kile ambacho anakwenda kukitafuta nje.
Kuna wanawake wengi wamekuwa wakiwanyanyasa wanaume kwa kauli zisizo
nzuri…kama jana nilikupa na leo unataka kwani mimi sichoki…nk. Ingawa
inaonekana kama ni suala lisilo na maana, lakini zungumza na wanaume wengi
ambao wametoka tayari nje ya ndoa, mojawapo ya sababu ni kutokuwa na uhakika wa
kushiba katika ndoa zao. Hawapati raha ile ambayo wanandoa wanastahili kupewa.
Kuna wanandoa wamekuwa wanaishi isivyo sawa, kwamba wanaishi bila kuelewana
vizuri. Kuelewana baina ya wanandoa ni suala la msingi sana. Matatizo mengi
ndani ya nyumba yanaweza kusababishwa na moja au baadhi ya tabia za baadhi ya
wanandoa, kwamba mwingine anakuwa hana ukaribu au anafanya mambo ambayo
hayamfanyi mmoja kati yao kutokuwa na amani moyoni.
Wanapoanza uhusiano mwanamke kwa mwanaume, hujali sana kuvaa vizuri, usafi
wa mwili wake, usafi wa nyumba na nidhamu ya hali ya juu. Aidha huwa ni kawaida
kwa mwanamke kumuuliza mwenzi wake anapenda kipikwe chakula gani na kadhalika.
Hata hivyo kadri siku zinavyokwenda mbele, si wanawake wengi huona umuhimu wa
kuwauliza wenza wao chakula cha kupika.
Wengi hupika chakula bila kuzingatia vionjo vizuri wala kuwa na ubunifu.
Wengine wamekuwa hawana mapokezi mazuri kwa wenza wao. Lini uliwahi kumpokea
mwenzi wako kwa kumpokea kwa kumkumbatia? Kila aliyeko kwenye ndoa anapaswa
kujiuliza hili.
Kuweni na mazungumzo
Mazungumzo ni njia muhimu ya kujenga ndoa na kuiimarisha , aidha ni njia ya
mkato ya kuchokana na kuchukiana. Mwanamke ambaye hajui wakati gani aseme nini
na wakati gani asiseme, hujikuta katika wakati mgumu ndani ya ndoa yake.
Kama una mwanamke wa namna hii ambaye kila anapoongea na mume wake huanza
mazungumzo yake na matatizo na lawama humfanya mumewe awe na woga kila
anaposikia sauti yake, na kuiona nyumba chungu, kwa sababu hakuna binadamu
anayependa kusikia matatizo tu wakati wote.
Ukweli mwanamke wa aina hii huwa anamsubiri mumewe kwa hamu kubwa, na
anapofika tu na kabla hata ya kupata rizki, anaanza kumsomea orodha ya
matatizo; watoto wamerudishwa shule, karo haijalipwa, shangazi yako amepiga
simu mjomba kalazwa Hospitali na kadhalika na kadhalika. Nyumba ya aina hii
huzeeka haraka na wanandoa kuchokana.