Simulizi ya Kusisimua Sehemu ya 4
Ilipoishia...
“We
mhudumu hembu njoo utoe hizi takataka zako hapa. Sisi tunakula nyie mnawaachia
machizi waje kutusumbua. Vipi bwana!” yule mzee alizungumza kwa ukali. Amakweli
umdhaniae ndiye kumbe siye. Kwa muonekano yule mzee alionekana ni mtu mtaratibu
sana na mwenye huruma kumbe ilikuwa kinyume.
Endelea…
Ayubu
aliona kuwa alikuwa amekwisha haribu pale ndani. Aliamua kuondoka kwenda
kufikiria cha kufanya. Wakati akiondoka alihisi mtu anamvuta shati.
“We kijana” yule mtu aliyemgusa aliita. Ayubu aligeuka pasipo kuongea kitu na
kukutana na mwanamke wa makamo.
“Shikamoo” Ayubu alisalimia.
“Marahaba. Vipi una tatizo gani?”
“Njaa mama” Ayubu alisema kwa hudhuni.
"Twende ukakae pale upate chochote” alisema yule mama na kuelekea pale
alipokuwa amekaa awali. Ayubu hakuweza kuamini kama amepewa jukumu la kuchagua
chakula alichokuwa akikitaka. Kutokana na njaa aliyokuwa nayo alijikuta akiagiza
ugali na maharage. Yule mwanamke aliamua kumuagizia chai na chapati kwasababu
kulikuwa ndio kwanza asubuhi. Chakula kilipofika Ayubu alikifakamia mithili ya
ng’ombe anayenyonya akatenganishwa na mama yake kwa muda mrefu halafu
wakakutanishwa tena. Yule mwanamke alimuangalia na kutingisha kichwa
kusikitika.
“Mimi naitwa Mama Suzy, naishi Kijitonyama pamoja na mumewangu na binti yangu”
“Mimi naitwa Ayubu”
“Unaishi wapi Ayubu?”
“Mnh! Kwakweli sina pa kuishi mamaangu”
“Unamaanisha wewe ni chokoraa?”
“Hapana……..ndio”
“Sasa mbona sikuelewi. Mara ndio mara hapana. Ok tuwachane na hayo, vp mbona
unavidonda usoni imekuwaje?” Mama Suzy aliamua kuachana na swali la kwanza
kwani aliamini kuwa jibu lingepatikana tu. Ayubu aliamua kuzungumza kila kitu
kilichomtokea tangu siku aliyofika pale jijini DareSalaam hadi siku ile. Mama
Suzy alijikuta machozi yakimtoka kutokana na yale aliyo yasikia.
“Pole sana kijana”
“Ahsante”
“Sasa utakwenda na mimi nyumbani kwangu” Mama Suzy alisema kwa huruma. Ayubu
alishituka baada ya kusikia taarifa zile. Aliinua macho na kumtazama yule mama
usoni. Akawa kama vile hajasikia vizuri.
“Naam!”
“Utakaa kwangu hadi utakapo mpata mwenyeji wako” alisema mama Suzy kwa mkazo.
Ayubu alivuta pumzi na kuzitoa nje kwa nguvu. Hakuamini masikio yake, alitaka
kupiga magoti ili kutoa shukurani zake kwa mama Suzy lakini mama Suzy alimuwahi
na kumzuia asifanye kitendo kile.
“Nashukuru sana mama. Mungu akubariki”
“Usijali mwanangu ni mambo ya kawaida. Maliza kula tuondoke” alisema mama Suzy
huku akifungua pochi yake na kutoa pesa za kulipia chakula. Ayubu alipomaliza
kula waliondoka pamoja kuelekea Kijitonyama.
****
Mama
Suzy alikuwa ni mke wa mzee Manyama. Walibahatika kupata mtoto mmoja tu wa kike
ambaye ndiye waliyempa jina la Suzy. Walikuwa wakimpenda sana binti yao huyo.
Mzee Manyama alikuwa akijitahidi kwa kadri ya uwezo wake kumtimizia kila
alichokuwa akikihitaji bintiye huyo ili asishawishike na majaribu ya kidunia.
Suzy alikuwa ni mwanafunzi wa kidato cha pili sawa na kidato alichoacha Ayubu
kule Lusanga.
Mama Suzy alipofika na Ayubu pale nyumbani alimkuta Suzy akifua sare zake za
shule. Alipomuona mama yake alimkimbilia na kumkumbatia kwa shangwe.
Alimsalimia na kumpokea mfuko mdogo wa rambo aliokuwa ameuning’iniza mkononi.
Suzy alimtazama Ayubu kwa macho yaliyojaa mashaka na chuki. Mavazi aliyokuwa
amevaa Ayubu yalikuwa yakimtafsiri kama chokoraa wa mjini ama chizi.
“Mama, huyu nani?” alihoji Suzy
“Huyu ni kakaako” alisema mama Suzy kwa ufupi.
Suzy
aliposikia jibu alilopewa na mama yake, aliangua kicheko ambacho kilipelekea
kukaa chini huku akiwa ameshikilia mbavu. Alikohoa mara kadhaa huku akiendelea
kucheka.
“Mama bwana. Yaani watu woote hukuwaona hadi kuleta haka kachokoraa halafu heti
unamwita kaka yangu. Ana hadhi ya kuwa kaka yangu huyu? Hembu mwangalie zile
nguo zake”
“Suzy shika adabu yako” mama Suzy alimfokea binti yake. Suzy alipobaini kuwa
mama yake alikuwa amekasirika, aliwacha kucheka na kumuomba msamaha. Suzy
alipeleka ndani ule mfuko aliompokea mama yake kisha akatoka nje na kuwaacha
Ayubu na mama yake ndani.
Ayubu alioneshwa bafuni na kwenda kujimwagia maji. Alipotoka alioneshwa chumba
ambacho angekitumia kulala na kubadirishia nguo. Kilikuwa ni chumba chenye
nafasi ya kutosha. Alipotupa macho kitandani aliona amewekewa nguo za
kubadilisha. Kumbe walivyotoka kule kwenye mgahawa walipitia Kariakoo kwanza na
kununua nguo kwa ajili ya Ayubu. Alivaa T-shirt na jeanse kisha akaenda
sebleni.
Alimkuta mama Suzy ameketi sebleni akichambua mboga kwa ajili ya chakula cha
mchana. Alipomuona Ayubu hakuweza kuamini. Kumbe Ayubu alikuwa ni kijana mzuri
sana ambaye uzuri wake ulikuwa umefichwa na matatizo. Mama Suzy alitoa tabasamu
na Ayubu naye alilipokea lile tabasamu na kutoa lakwake.
‘Umependeza sana Ayubu” alisema mama Suzy.
“Ahsante mama” Ayubu alijibu huku akiketi kwenye kochi pale sebleni. Mama Suzy
alipaza sauti na kumuita mwanae ambaye bado alikuwa akiendelea kufua. Suzy
alitegemea kuwa akiingia tu angemkuta yule chokoraa ameketi kwenye kochi
alilonunua baba yake. Alipanga kuwa endapo angemkuta ameketi kwenye kochi
asingemhofia mama yake, bali angemtimua kama mbwa.
Suzy alisimama mlangoni huku akizunguusha macho pale sebleni. Alikuwa
akimtafuta yule chokoraa aliyeingia na mama yake. Kwenye kochi alimuona kijana
mtanashati, mzuri, na mwenye mvuto. Hakujua kijana yule aliingia saangapi
kwasababu yeye alikuwa akifua nguo karibu na mlango, hivyo kama angeingia mtu
ni lazima angemuona. Alivuta pumzi na kuzitoa kwa nguvu.
“Mama yule Chokoraa wako yuko wapi?” Suzy alihoji kwa kiburi.
“Suzy, hivi kwanini hutaki kusikia?”
“Sio hivyo mama. We unatuletea machizi humu ndani!”
“Hembu kaa hapo. Nimekuita” mama Suzy alitoa amri na Suzy aliitekeleza.
Aliingia na kuketi pembeni mwa kijana mtanashati. Alimtupia jicho la pembeni
ili kumthaminisha. Alihisi mapigo yake ya moyo yakimuenda mbio. Hakujua ni
kwanini alikuwa vile, lakini hiyo ndiyo ilikuwa hali halisi.
“Suzy mwanagu, huyu anaitwa Ayubu. Ni kaka yako” alisema mama Suzy huku
akitarajia kuwa Suzy angeleta upuuzi kama wa awali.
“Anhaa karibu kaka Ayubu”
“Nashukuru sana”
“Ayubu, huyu ni dada yako anaitwa Suzy. Mtakuwa pamoja mkisaidiana hili nalile”
alisema mama Suzy na kupelekea Suzy kulipukwa na furaha. Akashindwa kujizuia
kuonesha furaha yake.
`
“Woow! Kwahiyo tutaishi wote hapa nyumbani?”
“Ndio hivyo. Naomba umpe ushirikiano”
“Sawa mama, hilo halina tatizo”
“umefurahi enh?”
“Sana. Lakini mama…”
“Enhee…”
“Hivi yule chokoraa uliyeingia naye yuko wapi?” Suzy alihoji kwa msisitizo huku
akiwa haelewi chokoraa aliyekuwa anamzungumza ndiye yule kijana mzuri
aliyetambulishwa na mama yake.
Endlea hapa>>
Endlea hapa>>