BONGO DAS'LAAM Sehemu ya 3
Ilipoishia....
“Hembu
lifunue” sauti ya mtu yule ilizidi kumshitua Ayubu na kumfanya atetemeke.
Alifahamu wazi kuwa watu wale waliokuwa na silaha zilizokuwa zimelowa damu,
wasingeweza kumuacha akiwa hai.
Ayubu
alifumba macho na kumuomba Mungu atende miujiza. Yule mtu aliyeambiwa afunue
tenga aliliangalia kitambo kisha akaligongagonga kwa ule mguu wake.
Endelea....
“Hakuna
sababu ya kulifunua. We weka mzigo tusepe”
“Basi
angalia kama kuna mtu anatuona”
“Hakuna
bwana, hembu wacha woga”
“Inabidi
kesho tuhakikishe mteja anapatikana” alisema yule mwengine na kutoa kifuko
kidogo na kukichomeka kwenye lile tenga. Alishituka baada ya kumgusa Ayubu
kwenye mgongo.
“Mnh!”
“Vipi?”
“Hapa
kuna mtu nini!”
“Kwani
vipi?”
“Kuna
kitu kigumu”
“Achana
nacho, weka mzigo wetu tuondoke. Mtu hawezi kakaa hapo”
Watu
wale baada ya kuficha kale kamfuko kao walielekea upande wa pili wa maeneo
yale. Ayubu alitulia kwa muda mrefu hadi alipobaini kuwa hapakuwepo na
mtu mahali pale. Alijitoa taratiibu kutoka kwenye lile tenga. Alichukua
kile kifurushi kilichokuwa kimefichwa na wale watu. Alipokifungua hakuweza
kuamini macho yake. Yalikuwa ni madini ya dhahabu, kitu ambacho kilimsababisha
kuwacha masomo na kwenda mgodini.
Hakutaka kuchelewa, alikitumbukiza kwenye nguo ya ndani na kuondoka haraka
kuelekea kule walikotokea wale watu. Akili yake ilikuwa ikiwaza utajiri.
Alijiona ni kiasi gani Mungu amempendelea kwa kumpa utajiri akiwa bado kijana
mdogo vile. Taswira ya jumba kubwa la kifahari na magari ya kifahari ilimjia
akilini mwake.
Alipata nguvu ya kutembea kwa muda mrefu ili kutafuta mahali pa kulala usiku
ule ambapo ni mbali na maeneo yale. Alikwenda kujilaza pembeni ya duka moja
kubwa la sonara. Aliamini maeneo yale pasinge kuwepo na mtu yoyote ambaye
angemfanyia kitu kibaya kwasababu palikuwa peupe. Hivyo ingekuwa rahisi kuomba
msaada hata kutoka kwa walinzi wa maduka.
Alitandika kirago na kujilaza, aligalagala kwa muda mrefu pasipo kupata
usingizi. Mara ilifika gari ya polisi na askari watu walishuka. Ayubu
alishituka na kutaka kukimbia kutokana na jinsi askari wale walivyoshuka kwa
mbwembwe kutoka kwenye gari. Walimzunguuka Ayubu na kuanza kuongea nae.
“We kijana, unafanya nini hapa”
“Nime….nime….nimejipumzisha Afande”
“Wewe ni mwizi”
“Ha…ha…ha…hapana”
“Msirichereweshe Afande. Rireteni turipereke. Riuaji hiro” alisema askari
aliyekuwa kwenye gari kwa msisitizo.
Ama
kweli “kama haipo haipo tu” kwenye lile duka la sonara alilokuwa amelala Ayubu,
kulikuwa kumevunjwa na kufanyika kitendo cha wizi. Mbaya zaidi watu walioiba
wamefanya mauaji ya mlinzi wa duka lile. Askari walianza kufanya upekuzi kwa
Ayubu. Laahaula! Alikutwa na kufuko cha dhahabu kwenye sehemu zake za siri.
“Haaa! We kijana kumbe ni rijambazi?”
“Jamani sio mimi”
“Hii umetoa wapi?”
“Nimeokota, lakini sio hapa”
“Pumbavu, umewezaje kuua peke yako au unawenzio?”
“Hapana mimi sijaua jamani” alilalamika Ayubu huku akilia kwa uchungu.
“Utaozea jera kunguni wee” alisema askari huku wakimnyanyua na kumtumbukiza
kwenye gari yao. Ayubu alipigwa virungu kwa kiasi kikubwa. Alijikuta nguvu
zikimuishia na kunyong’onyea kutokana na kipigo kile kitakatifu. Ingawa alilia
sana na kuomba asamehewe lakini sauti yake haikusikika na hata askari mmoja.
Gari ilikuwa ikienda kwa mwendo wa kasi sana. Ilikuwa ikielekea kituo kikuu cha
Ostabey. Laahaula! Mkosi ndani ya mkosi, kulitokea gari la mchanga ambalo
halikuwa na taa na kulivaa lile gari la polisi. Walibingirika mara tatu
na mwisho gali ilisimama matairi yakiwa juu. Ayubu alijua amekwisha
poteza maisha. Lakini haikuwa hivyo kwani alitingisha mkono, mguu, na
kuchezesha macho bila matatizo. Maumivu aliyokuwa akiyasikia yalikuwa ni yale
ya virungu. Kwa ufupi ni kwamba hakuwa ameumia hata kidogo kutokana na ile
ajali.
Siku zote ajali ni kitu kibaya sana, lakini siku ile kwa Ayubu ilikuwa kinyume.
Alimshukuru mungu kwa kuwasababishia ajali ile. Askari wote walikuwa wamepoteza
maisha pale pale. Alichokifanya ni kujichomoa na kuketi hatua kadhaa kutoka
pale kwenye ajali. Alishuhudia maiti za askari zikichomolewa na kupakiwa kwenye
gari la kubebea wagonjwa.
Pale alipokuwa amekaa Ayubu alihisi mtu anamgusa kwenye bega lake la kushoto.
Alipogeuka akahisi mapigo ya moyo yakimwenda mbio. Alikuwa ni mmoja wa wale
watu waliokuwa wameficha dahahabu zao kule kwenye uchochoro.
“Habari yako” Mtu yule alitoa tabasamu na kumsalimia Ayubu.
“Safi tu, niaje?”
“Shwari”
“Nawewe ulikuwepo kwenye ajali?”
“Amm….ah…hapana sikuwepo”
“Najua ulikuwepo kwasababu nimekuona ukitoka”
“Umenifananisha”
“Sikiliza kijana, ukileta uhuni nawaambia watu wakupeleke polisi. Sema kwanini
walikukamata?”
“Aaah! Wamenionea tu. Lakini sio mimi”
“Wamekuonea nini”
“Heti nimeu…..ah! sijui nimevunja duka”
“Umeiba nini?”
“Wanasema nimeiba madini”
“Yako wapi?”
“Amebaki nayo afande mmoja kwenye gari”
“Kweli?”
“Ndio” alijibu Ayubu na kumfanya kijana yule kwenda kwa kasi kwenye lile gari
lililopata ajali. Ayubu aliutumia mwanya ule kuondoka maeneo yale. Alihisi kama
angeendelea kubaki pale angeweza kutokea mwengine na kumpeleka polisi.
****
Hadi
kulipo pambazuka Ayubu alikuwa akitembea. Siku hiyo hakupata kabisa hamu ya
kulala tena. Alihisi kuwa ni lazima angeingia mikononi mwa polisi ama vibaka wa
jijini kama angelala. Alikuwa ametembea umbali mrefu kutokea pale alipopata
ajali usiku. Alikuwa amefika maeneo ya Ubungo.
Njaa ilikuwa ikimuuma sana kwasababu tangu chakula alichokula mchana siku
iliyopita hakutia kitu kingine mdomoni mwake. Aliwaza kitu cha kufanya asubuhi
ile ili apate chochote cha kutia mdomoni. Alisogea hadi karibu na mgahawa mmoja
uliokuwa karibu yake. Aliingia na kuwakuta watu wakiagiza na kupata kifungua
kinywa. Alimfuata mzee mmoja aliyekuwa amekaa kwenye kona. Mzee yule alionekana
kuwa na roho nzuri na sura ya huruma.
“Shikamoo mzee”
“Marahaba hujambo?”
“Samahani mzee wangu”
“Unasemaje?”
“Tangu
jana sijala naomba unisaidie nipate chochote mzee wangu”
“Sina hela mimi. Unadhani pesa zinaokotwa?”
“Nisaidie mzee wangu”
“We mhudumu hembu njoo utoe hizi takataka zako hapa. Sisi tunakula nyie
mnawaachia machizi waje kutusumbua. Vipi bwana!” yule mzee alizungumza kwa
ukali. Amakweli umdhaniae ndiye kumbe siye. Kwa muonekano yule mzee alionekana
ni mtu mtaratibu sana na mwenye huruma kumbe ilikuwa kinyume.