Upinzani nchini Tanzania umetia saini
makubaliano ya pamoja, kuking’oa madarakani Chama tawala.
Utiaji huo saini makubaliano ya kukishinda
Chama cha Mapinduzi CCM, katika uchaguzi ujao, umefanywa na viongozi wa vyama
vinne, huku tukio hilo likishuhudiwa na wafuasi wao.
Katibu Mkuu wa Chama kikuu cha upinzani
CHADEMA, Dr. Willibrod Slaa ni miongoni mwa viongozi waliotia saini makubaliano
hayo na amesema vyama hivyo vitasimamisha wagombea wake kwa pamoja kwenye ngazi
zote za uchaguzi kuanzia serikali za mitaa mpaka ngazi ya urais.
Katibu mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim
seif Sharif Hamad anasema tukio hilo la vyama kusaini makubaliano ya kufanya
kazi kwa pamoja kwa lengo la kuing’oa CCM ni muhimu na la kihistoria.
Viongozi waliotia
saini waraka huo wa makubaliano ni Freeman Mbowe Mwenyekiti wa chama kikuu cha
upinzani CHADEMA, Profesa Lipumba Mwenyekiti wa Chama cha wananchi CUF, Katibu
Mkuu wa Chama hicho ambaye pia ni Makamu wa kwanza rais wa Zanzibar Maalim Seif
Sharif Hamad, James Mbatia Mwenyekiti NCCR Mageuzi, Mosena Nyambabe Katibu Mkuu
NCCR Mageuzi, Dr Emmanuel Makaidi Mwenyekiti NLD na Tozzi Matwanga Katibu Mkuu
wa NLD
Chanzo BBC