Ni baada ya Waziri Mwanri kusema kama
viongozi wakikataa watoto kupewa mimba, tatizo hilo litakwisha.
Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Martha
Mlatha amemtaka Naibu Waziri wa Nchi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Aggrey Mwanri kuwaomba radhi wasichana nchini nzima kwa
kuwadhalilisha.
Mbunge huyo alitoa kauli hiyo bungeni jana
alipouliza swali la nyongeza.
“Uwatake radhi wasichana wote kwa
kuwadhalilisha. Unasema kama wenyeviti wa Serikali za Mitaa wakikataa kuwa
watoto huwa ‘hawapigwi’ mimba, itawezekana kupunguza mimba za utotoni. Viongozi
wangapi kuanzia ngazi ya Taifa ambao wamechukua hatua kwa watoto waliopata
tatizo hilo?” alihoji.
Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia alisema suala la kuzuia mimba za utotoni
ni la watu wote.
“Ukitembea barabarani unakutana na vibinti
vidogo vinatembea saa 2.00 usiku. Maeneo mengine kuna sheria zinazokataza
watoto wadogo kuingia katika vibanda vya sinema,”alisema.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti
Maalumu (CCM), Riziki Said Lulida alihoji kwamba Serikali ina mkakati gani wa
kutatua tatizo la mimba za utotoni kwa kuwa Lindi inaongoza kwa tatizo hilo,
hali inayosababisha kufanya vibaya katika sekta ya elimu.
Akijibu, Mwanri alisema Serikali imekuwa
ikihamasisha jamii kufuatilia mahudhurio ya watoto wao shuleni.
Alisema imeboresha somo la elimu rika kwa
kutoa elimu ya afya ya uzazi inayoendana na makuzi.
Naibu Waziri Mwari alisema watu
wanaobainika kuwakatiza masomo watoto au kuwashawishi kuingia katika mahusiano
ya kimapenzi, huchukuliwa hatua za kisheria .
Chanzo: Mwananchi