Ikulu imekana kuwapo kwa njama zozote za kutaka kumuangamiza Mwenyekiti Mtendaji wa IPP Dk. Reginald Mengi Zilizodaiwa kuandaliwa na Rais Jakaya Kikwete kwa kile kilichodaiwa kuwashughulikia wanaoihujumu serikali yakee na kupanga kumshughulikia.
Njama hizo ziliripotiwa na baadhi ya
vyombo vya habari, ambavyo vilidai kunasa mazungumzo kati ya Rais Kikwete na
Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, ambaye anadaiwa kumchongea
Dk. Mengi kwamba, ndiye kinara anayesababisha serikali yake iyumbe kila mara.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Ikulu, Salvatory Rweyemamu, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Rais
Kikwete hawezi kushiriki katika njama za kumdhuru raia na kwa hiyo, habari hizo
ni za kutengenezwa kwa nia mbaya ya kutaka kuharibu urafiki uliopo kati ya Rais
na Dk. Mengi.
Alisema Rais Kikwete alizisikia
habari hizo akiwa nchini Jordan, Jumamosi ya wiki iliyopita na kushangazwa
nazo.
Hata hivyo, alisema Zitto, ambaye
ndiye wa kwanza kushutumiwa kuhusiana na habari hizo alikwishazijibu kwa kuzikanusha
na kwamba, juzi Dk. Mengi alihudhuria sherehe za kutunuku nishani Ikulu, hivyo
haamini kwamba, mahali pabaya kiasi hicho, ambako kuna watu wanamsubiri ili
kumdhuru, anaweza kwenda.
Alisema madai kwamba, Zitto na Rais
Kikwete walikutana Ikulu na kuzungumzia suala hilo, hayana ukweli, kwani hakuna
mkutano wa ana kwa ana au mazungumzo ya simu, yaliyofanyika kati ya viongozi
hao wawili katika miezi ya hivi karibuni.
“Hata wakati huo, ambao ingetegemewa
wangewasiliana labda kwa namna ya mazingira ya wakati huo wa matatizo ya Escrow
na nini na nini, hawakuwasiliana kwa sababu Rais alikuwa anatibiwa nje ya nchi.
Kwa hiyo, hapakuwapo na mkutano wa namna hiyo wa mbinu sijui za kupanga mbinu
za kumuumiza mtu,” alisema Rweyemamu.
Alisema pia Rais huapa kulinda raia
wote na mali zao, hivyo hawezi kugeuka na kuanza kula njama za kujaribu
kumdhuru raia yeyote nchini.
Rweyemamu alisema pia Rais Kikwete
na Dk. Mengi huwasiliana sana, kwani anayo simu yake na amekuwa akimpigia mara
nyingi na kuzungumza naye, hivyo alidhani busara bora zaidi kwenye jambo hilo,
ingeongoza kwamba, Dk. Mengi angempigia Rais na kutaka kujua ukweli kuhusiana
na habari hizo.
“Wakazungumza wote wawili, watu
wazima, wazee wenye busara sana wakaelewana, kwamba tumeliruhusu hili suala
kutoka pale lilipotakiwa kuja, tukalitumbukiza kwenye ukumbi wa kila mtu wa
hadhara inakuwa jambo gumu kidogo kueleweka,” alisema Rweyemamu.
Aliongeza: “Ndio maana nikasema
tulipopata habari, sisi hatukujua tu-react (tujibu) vipi. Yaani kwa sababu jambo
halipo, jambo limetungwa, limefinyangwa finyangwa hivi likatupwa hivi mbele ya
watu, hatujui limeanzia wapi. Hata unapoiambia Ikulu, Kurugenzi ya Mawasiliano
sijui, Mkurugenzi wa (Idara ya) Habari (Maelezo) hawakujibu. Tujibu nini?
Hatujui. Kwa hiyo ndio maana sasa tukaanza sasa kuwasiliana jamani kuna hili
tufanye nini? Tena kuna watu wengine walikuwa wanasema bwana hata ukiulizwa
usiliseme. Kwamba, ni jambo halipo, halina maana, tuachane nalo lipite.”
Hata hivyo, alisema jana alilazimika
kulizungumzia kwa kuwa aliulizwa na waandishi wa habari, pia kwa vile
anayeshutumiwa ni Rais na shutuma zinahusu usalama wa raia wake, hivyo alifanya
hivyo ili wananchi wapate kupumua japo kidogo.
Chanzo NipasheMATUKIO ZAIDI YA KUSISIMUA BOFYA HAPA>>