Waziri wa Habari, Utamaduni, Michezo na Wasanii, Nape Nnauye,
amewasimamisha kazi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Matukio wa Shirika
la Utangazaji la Taifa (TBC), Mbwilo Kitujime na Meneja wa Vipindi wa
shirika hilo, Edna Rajab.
Nape alitoa uamuzi huo alipofanya ziara katika ofisi za shirika hilo zilizoko Mikocheni jijini Dar es Salaam jana.
Pia, aliagiza kufumuliwa kwa idara nzima ya habari na matukio ya TBC kutokana na utendaji usioridhisha.
Aidha, wakati Nape akifikia uamuzi huo, Waziri wa Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, naye amemwagiza
Mwenyekiti wa Bodi ya Bohari ya Dawa (MSD), Prof. Idrisa Mtulia,
kuwasimamisha kazi mara moja wakurugezi wanne wa bohari hiyo kwa tuhuma
za upotevu wa Sh. bilioni 1.5, akiwamo aliyekuwa Kaimu Mkurungezi,
Cosmas Mwaifwani.
Wengine waliosimamishwa ni Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, Joseph
Tesha, Mkurugenzi wa Ugavi, Misangi Muja na Mkurugenzi wa Manunuzi,
Heri Mchunga.
Waziri Ummy alisema uamuzi huo umechukuliwa baada ya uchunguzi
uliofanyika mwaka jana kubaini taratibu za manunuzi zilikiukwa na
kuisababishia serikali hasara.
Kauli hiyo aliitoa jana katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
alipokuwa akipokea vitanda 120, magodoro 120, vitanda vya kujifungulia
10, vitanda vya watoto njiti 10 na mashuka 420 kutoka kwa Mkurungezi
Mkuu wa MSD, Laurean Rugambwa Bwanakunu.
Makabidhiano hayo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli
kuwa jengo lililokuwa likitumika kama Ofisi ya Kitengo cha Uzazi na
Mtoto litumike kuwa wodi ya wazazi Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Pamoja na kupokea vifaa kwa ajili ya wodi ya wazazi, lakini pia
viongozi hao lazima wasimamishwe haraka ili kupisha uchunguzi
ufanyike, hata wafadhili wamesimamisha kutoa fedha za kununulia dawa
kutokana na upotevu huo wa fedha,” alisema.
Aliongeza kuwa, kabla yeye hajaondoka katika nafasi yake ya
uwaziri, wote watakaobainika kufanya uzembe kwenye manunuzi ya dawa na
vifaa tiba baada ya uchunguzi wachukuliwe hatua.
Wakati huo huo, waziri huyo aliwaangiza wakuu wa mikoa na wilaya
kuhakikisha wanapokea taarifa ya idadi ya vitanda na wagonjwa wanaolala
chini kila siku kutoka hospitali za wilaya na mkoa ili hatua
zichukuliwe haraka.
“Namshukuru Rais John Magufuli kwa kutoa msukumo katika wizara
ninayosimamia, mimi na Katibu Mkuu Dk. Mpoki Ulisubisya, hatutalala
lazima tutahakikisha taarifa zinapatikana kila siku kutoka hospitali
zote nchini,” alisema.
“Rais anapotoa agizo hapendi kusikia mchakato, upembuzi yakinifu
unafanyika, bali hupenda kuona hatua zinachukuliwa mara moja, hivyo
wajawazito wanahamia leo (jana) katika jengo ambalo Rais alihitaji
litumike.”
Alisema wafanyakazi wote waliokuwa wakifanya kazi katika jengo
lililokuwa MNH, watapelekwa kwenye mamlaka nyingine, ikiwamo Mamlaka ya
Chakula na Dawa Tanzania (TFDA).
Awali, akikabidhi vitanda na magodoro kwa Waziri wa Afya,
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Rugambwa alisema wametekeleza agizo la Rais
Magufuli la kupeleka vitanda katika jengo lililokuwa likitumiwa kama
ofisi na wafanyakazi wa Wizara ya Afya.
“Tumeanza kuleta vitanda na mashuka kwa lengo la kupunguza
changamoto ya wajawazito kulala chini katika wodi ya wazazi,” aliongeza
kusema.
Chanzo: Nipashe