Wanafunzi wa Chuo cha Ualimu wa elimu maalumu Patandi mkoani Arusha jana walifanya vurugu zilizowalazimisha Polisi kuwasambaratisha kwa mabomu.
Mh Kawambwa
Wanafunzi waligoma na kufunga
barabara kuu ya kutoka Moshi -Arusha kwa kutumia mawe kwa takribani saa moja
kuanzia saa 4 hadi 5 asubuhi.
Wakizungumza wanafunzi hao walisema lengo la mgomo wao ni kushinikiza mkuu wa chuo
aondolewe.
“Chanzo cha vurugu hizi ni kufikisha
kilio chetu kwa ngazi za juu,” alisema mwanafunzi mmoja.
Alidai mkuu wa chuo hicho Zaina
Mbelwa, anawapa adhabu za shule za msingi kama kuwapigisha magoti, kuwapiga
makofi na kuwafanyisha usafi wakati wanatoa Sh. 30,000 za kufanyiwa usafi.
Mkuu wa Polisi wa Kituo cha Usa River,
Msolo Msolo, alisema walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya
wanafunzi na kutuliza hali ya hewa.
Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa
Chuo Mbelwa, alisema wanafunzi hao walifanya hivyo kwa sababu ya kuwabana ili
wafuate sheria na kanuni za chuo.
Alisema baadhi ya wanafunzi wanavuta
bangi na kutumia dawa za kulevya na hivyo kuvunja sheria na kanuni za chuo.
Pia alisema baadhi yao wanajiingiza
katika mahusiano ya kimapenzi na walimu badala ya kufuata masomo na pale
wanapolazimika kuwakagua wanagoma.
Kuhusu fedha za usafi, alisema
wanalipa Sh. 15,000 na sio Sh. 30,000 kama wanavyodai.
Alikiri kuwaadhibu wanafunzi
wanaokiuka sheria na kanuni tena wengine hawahudhurii masomo na badala yake
wanasikiliza redio.
Kuhusu chakula, alisema kuna tatizo
ambalo sio lake, ni la mzabuni ambaye amegoma kuleta mboga akidai hajalipwa Sh.
milioni 220 za mwezi Machi.
Akizungumzia kuhusu uongozi wa
wanafunzi, alisema wanafunzi hao hawana uongozi na ndio maana tatizo hilo
limejitokeza.
Katika mazungumzo na polisi jana,
walimshauri kuitisha uchaguzi wa viongozi wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo
mapema.
Alisema baada ya kumaliza mitihani
siku tano zijazo, ataitisha uchaguzi.
Baadhi ya walimu walisema kwa
nyakati tofauti kuwa mkuu wa chuo ndio tatizo.
Walidai mwa mfano, mkuu wa
chuo ndiye afisa masurufu na ndiye anayesaini akaunti za shule na pia
amewatenga walimu na kila kitu anafanya mwenyewe.
Walidai pia amekuwa akiwagawa
kikanda, dini pale safari zenye kulipwa marupurupu zinapopatikana.
Walisema kilio hicho kimefikishwa
ngazi nyingi ila hawasilikilizwi na matokeo yake walimu wanahoji wanaitwa
Ukawa.
(Ukawa ni Umoja wa Katiba ya
Wananchi ambao ulianzishwa na vyama vya upinzani katika kipindi cha Bunge
Maalum la Katiba kupinga mchakato huo).
Chanzo Nipashe