Mapigano yameibuka tena kati ya wafugaji wa kijiji cha Kambala na Mkindo, wilayani Mvomero na kusababisha vifo vya watu wawili na kujeruhi wengine watatu.

Mapigano hayo ya kushambuliana kwa sime na mikuki yenye sumu kali, yalitokea juzi  jioni na chanzo chake kimeelezwa kuwa ni ng’ombe wa wafugaji kuingizwa katika mashamba ya wakulima katika Bonde la Mgongola ambalo limekuwa likigombewa baina ya pande hizo mbili.

Taarifa kutoka eneo la tukio zinaeleza kuwa wakulima walitaka kuwaondoa ng’ombe hao na hapo kukatokea kutoelewana ambapo wafugaji hao waliamua kumkata kwa sime mmoja wa wakulima hao.

Chanzo hicho kilieleza kuwa wakulima waliamua kujikusanya na kuita kundi la sungusungu maarufu kama ‘mwano’ na kwenda kuvamia katika kijiji cha wafugaji  ambapo walimkuta mfugaji mmoja akiwa na ng’ombe na alipowaona wakulima hao aliamua kukimbia kitendo kilichowafanya wakulima hao kuchukua ng’ombe zaidi ya  304 na kuanza kuwaswaga.

Hata hivyo, wakati wakiwaswaga, njiani walikutana na kundi la wafugaji na kuanza mapigano yaliyosababisha watu wawili kufariki dunia baada ya kupigwa sime na mapanga huku wengine watatu wakijeruhiwa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja waliokufa kuwa ni Kipasisi Kashu (19), mkazi wa kijiji cha Kambala na Shukuru Juma(23),  mkazi wa Kigugu katika kata Hembeti.

Alisema chanzo cha mapigano hayo ni ng’ombe wa wafugaji kula mazao ya shamba la Ignas Ramadhani.

Alisema majina ya majeruhi hayajapatikana lakini wanapatiwa matibabu katika hospitali ya Bwagala.

Alisema katika mapigano hayo mfugaji huyo alichomwa mshale wenye sumu begani na kufariki huku mkulima akikatwa na sime kichwani.
Chanzo Nipashe
 
Top