Hayo yalisemwa juzi na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Arumeru, Matias Manga kwenye kikao kilichowashirikisha viongozi hao wa Serikali za Mitaa na vijiji wa Kata ya Mlangarini.


Arumeru. Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Arumeru, imewaonya viongozi wake waliochaguliwa kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Jimbo la Arumeru Magharibi kama watahusika kuuza ardhi kinyume na sheria, haitasita kuwatimua.
      Hayo yalisemwa juzi na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Arumeru, Matias Manga kwenye kikao kilichowashirikisha viongozi hao wa Serikali za Mitaa na vijiji wa Kata ya Mlangarini.
Manga ambaye pia ni Diwani wa Kata hiyo, alisema CCM haitawavumilia viongozi walarushwa, wazembe na wanaosababisha migogoro ya ardhi wilayani humo.
       “Hatupendi kuona migogoro ya ardhi kila kukicha ikiendelea, kuna baadhi ya viongozi mnashiriki kuuza ardhi kwa kupewa asilimia ya mauzo na wanunuzi, mnasababisha migogoro, atakayebainika atakiona,” alisema.
Alisema baadhi ya matatizo wilayani humo yanasababishwa na viongozi wa ngazi za chini na lawama zinawakumba viongozi wa ngazi ya juu.
Alisema migogoro ya ardhi inayoendelea kutokea kwenye maeneo hayo, inapaswa kukomeshwa.
      Manga alisema hivi karibuni, baadhi ya watu waliwashutumu baadhi ya viongozi wa CCM kuwa walishiriki kuuchochea kwa lengo la kuficha uovu wao.
“Hatutakubali, lazima suala hili sasa lifike mwisho, mkianza ninyi huku chini sisi tutawamaliza huku huku chini msiwasingizie viongozi wa ngazi za juu,” alisema.
      Manga aliwataka viongozi ambao hawakuchaguliwa na walikuwa viongozi awali, kukabidhi ofisi kwa wakati ili kazi ziendelee kwa viongozi wapya. CCM imefanikiwa kushinda nafasi za mwenyekiti na watendaji wa vijiji katika maeneo mengi ya vijiji vya jimbo hilo.
Hata hivyo, ilijikuta ikipigwa mweleka na upinzani katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Ngaramtoni..
 Mwananchi
 
Top