Wanafunzi wa shule ya msingi Lukole iliyopo kata ya Negero tarafa ya Kimbe wilayani Kilindi wamekufa baada ya kusombwa na maji ya mvua wakati walipokuwa wakijaribu kuvuka ng'ambo
ya pili kwa kuogelea ndipo walipozidiwa na hatimaye kufa maji.
Akielezea tukio hilo, kamanda
wa polisi mkoani Tanga kamishna msaidizi wa jeshi hilo Zubeir Mwombeji amesema
limetokea katika kijiji cha Lukole kilichopo kata ya Negero wilayani Kilindi
ambapo wanafunzi hao jamii ya wafugaji walikuwa na mifugo ndipo waliposhawishiana
kuvua nguo zao ili waweze kuogelea hadi ngambo ya pili ndipo walipozidiwa hadi
kufa maji.
Katika hatua nyingine, watu
watatu wakazi wa jiji la Tanga na Dar es Salaam, wametiwa mbaroni na jeshi la
polisi baada ya kupatikana na shehena ya dawa za kulevya aina ya Mirungi zaidi
ya kilo 530 ambazo zilikuwa zikitokea nchi jirani ya Kenya kwenda jijini Tanga
kwa ajili ya kusambazwa kwa mawakala wa biashara hiyo.
Kamanda wa polisi mkoani Tanga kamishna msaidizi
wa jeshi hilo Zubeir Mwombeji amewataja watuhumiwa kuwa ni Mohamed Omary mkazi
wa barabara ya 14 jijini Tanga, Haruna Hamis
mkazi wa Tamta jijini Tanga na Aziz Athuman mkazi wa Dar es Salaam ambao wote
kwa pamoja wamekamatwa katika eneo la mpirani lililopo kata ya chongoleani,
tarafa ya chumbageni jijini Tanga.
CHANZO: ITV