Muuguzi mmoja wa zahanati ya Muungano, Chamwino mkoani Hapa, amekumbwa na kashafa nzito baada ya kudaiwa kumchapa viboko mama mjamzito wakati akiwa katika hali ya uchungu wa kujifungua na kusababisha mtoto aliyetaka kujifungua kufariki akiwa tumboni.
Aidha, mama huyo ambaye kwa sasa amelazwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, hali yake inaelezwa kuwa mbaya.


Mwanamke huyo, Mariamu Maroda, anadaiwa kulazwa kwenye chumba hicho kwa zaidi ya wiki moja, ambapo pamoja na kufanyiwa upasuaji, hakufanikiwa kupata mtoto wake akiwa hai.


Akisimulia mkasa huo, mama mdogo wa Maroda, Joyce Charles, alisema Aprili 3, mwaka huu Saa 12:00 jioni, walimpeleka zahanati ya Muungano akiwa na dalili za kujifungua na kupokelewa na muuguzi aliyemfahamu kwa jina la Lucy. “Nilishuhudia Lucy akimchapa Maroda viboko kwenye mapaja na mgongoni, akisema ana uwezo wa kujifungua lakini anadeka tu, nilishindwa kuingilia nikihofia asimdhuru zaidi mwanangu, ila nilihuzunika sana,” alisema.


Alisema muuguzi huyo alitumia fimbo tatu kumchapa mgonjwa wake, ambazo alikuwa akizitumia kila moja inapovunjika. Alisema fimbo hizo zilipomalizika, alianza kumfinya kwenye mapaja kwa kutumia rula.


“Kesho yake saa 12:00 alfajiri, huku hali ya mgonjwa ikiwa mbaya, walitupatia gari likatupeleka hospitali ya Mvumi Misheni, ambako walisema hali aliyokuwa nayo mgonjwa wasingeiweza na kutuelekeza tumpeleke hospitali ya rufaa, lakini walimpa mgonjwa chupa mbili za damu,” alisema.


Alisema Maroda alifikishiwa chumba cha upasuaji na kisha alilazwa wodi namba 17, lakini miguu na tumbo vilianza kuvimba na alipochunguzwa ikabainika ana usaha tumboni, hivyo aliamriwa arudishwe kwenye chumba cha upasuaji. “Yaani ukimuona, mwilini ana alama za fimbo na kufinywa. Sasa walipomfanyia upasuaji kwa awamu ya pili, alipelekwa ICU mpaka hivi tunavyozungumza ni zaidi ya wiki moja,” alieleza Charles.


Viongozi wa Hospitali ya Rufaa, wenye mamlaka ya kuzungumzia suala hilo walionekana ‘kurushiana mpira’ walipotakiwa kuelezea suala hilo. Hata hivyo, Muuguzi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anatoria Mkindo, alikiri kuwepo kwa mgonjwa huyo.


Awali Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Zainab Chaula, alisema hakuwa na taarifa za kina kuhusu Maroda.

Mkindo alisema walikuwa wameagiza Ofisi ya Mganga wa Wilaya wa Chamwino, kuwapelekea taarifa kuhusu suala hilo.


Alisema pia wametaka Ofisi ya Mganga Mkuu wa mkoa, ifahamishwe hatua zilizochukuliwa dhidi ya mtumishi aliyedaiwa kumchapa viboko mjamzito huyo.


“Mimi sio msemaji, anayetakiwa kuwapa taarifa kamili ni RMO (Chaula) kwanini awalete kwangu, nilichowaeleza ni ambacho nafahamu lakini siyo msemaji, nashauri muende ofisini kwa matroni wa hospitali mtapata taarifa kamili,” alisema.


Afisa Muuguzi wa ICU, Christina Mlumba, alisema, Maroda alipelekwa ICU baada ya kufanyiwa upasuaji na kwamba hali yake inaendelea vizuri.


Mdogo wa Maroda, Silika Mkwawi alivieleza vyombo vya habari kuwa ingawa hakuingia kwenye chumba cha kujifungulia katika zahanati ya muungano, dada yake alipotolewa nje, muuguzi alimueleza kuwa alimchapa fimbo mbili tu, kwa sababu ya kudeka kwake. 

 Chanzo Nipashe
 
Top