Msiba
mwingine mkubwa umelikumba taifa letu kwa kupoteza wananchi wake 38
katika matukio mawili tofauti likiwemo linalohusisha basi dogo aina ya
Toyota Hiace ambayo imeua watu 19 wakati ilipokuwa ikifanya safari zake
kwa wizi mkoani Mbeya.
Tukio
jingine limetokea mkoani Shinyanga ambako wachimbaji wadogo 19 wa dhahabu
waliokuwa katika mgodi mdogo wa Kalole, wilayani Kahama wamekufa baada ya
kufunikwa na kifusi usiku wa kuamkia jana kutokana na mvua kubwa zinazoendelea
kunyesha.
Picha hii si halisi
Matukio
hayo ni mwendelezo wa majanga ya ajali ambazo zimekuwa zikitokea kwa takriban
wiki mbili mfululizo na kuua mamia ya watu. Zaidi ya watu 980 wamefariki dunia
katika ajali za barabara katika muda wa zaidi ya miezi mitatu.
Katika
ajali ya basi iliyotokea saa 3:00 asubuhi jana katika Barabara ya Mbeya-Kyela
eneo la Kiwira ambalo ni maarufu kwa jina la Uwanja wa Ndege kutokana na magari
mengi yanayopata ajali kuonekana kama ndege inayoelekea kutua wakati
yakitumbukia kwenye bonde ambalo Mto Kiwira unapita, watu 18 walifariki papo
hapo na mwingine mmoja alifariki dunia akiwa Hospitali ya Igogwe.
Dereva
wa basi hilo, lililokuwa likipeleka wafanyabiashara kwenye gulio la Kiwira
wilayani Rungwe, alikuwa ameamua kufanya safari hiyo badala ya ruti zake za
kawaida za kuzunguka mjini Mbeya, baada ya madereva wa mabasi aina ya Toyota
Coaster kuwa na mgomo wa kupinga wenzao kupigwa faini kubwa.
Akizungumzia
ajali hiyo jana, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Zainab Mbiro alisema chanzo chake ni
mwendo wa kasi katika eneo lenye mteremko ambao una kona kali iliyo takriban
kilomita nne kabla ya kuingia Kiwira.
Eneo
hilo linajulikana kwa ajali nyingi ambazo zimekuwa zinachukua maisha ya watu
wengi kila mwaka.
“Basi
dogo limetumbukia kwenye Mto Kiwira baada ya dereva kushindwa kukata kona kutokana
na kuwa kwenye mwendo kasi katika eneo la mtelemko mkali maarufu kwa jina la
Uwanja wa Ndege,’’ alisema.
Eneo
hilo la urefu wa kilometa nane za barabara ya kuanzia Uyole kwenda Rungwe,
limewekewa vibao vya alama za tahadhari kwa madereva kuwatahadharisha kuwapo
kwa miteremko na kona kali.
Kamanda
wa polisi wa Mkoa wa Mbeya, Hemed Msangi, akiwa eneo la tukio jana, alisema
ajali hiyo iliua watu 18 palepale na mmoja alifariki dunia akipatiwa matibabu
kwenye Hospitali ya Igogwe, Kiwira na kwamba watatu walijeruhiwa na wamelazwa
hospitalini hapo.
Msangi
alisema maiti 18 zilipelekwa Hospitali ya Makandana wilayani Rungwe na mmoja
alibaki Igogwe. Hata hivyo alishindwa kutaja majina akisema karibu wote hawana
vitambulisho.
“Kibaya
zaidi ni kwamba gari lililopata ajali ni daladala linalosafiri kati ya Igawilo
na Majengo na wafanyakazi wake waliamua kuwachukua wafanyabiashara waliokuwa
wakienda kwenye gulio la Kiwira wilayani Rungwe baada ya (Toyota) Coaster
kugoma,” alisema.
Mabasi
hayo aina ya Toyota Coaster ndiyo yanayofanya safari kati ya mji wa Uyole na
Tukuyu.
Ajali
hiyo inafanya idadi ya waliokufa kati ya Januari Mosi na Aprili 12 mwaka huu
kufikia 988, kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa Kamanda Mpinga hivi karibuni.
Kamanda
Mpinga alisema watu 866 walikufa na wengine 2,363 kujeruhiwa kati ya Januari na
Machi, wakati wengine 103 wamepoteza maisha na 138 kujeruhiwa kati ya Machi 11
na Aprili 12 mwaka huu.
Kuhusu
mgomo wa mabasi aina ya Toyota Coaster, Kamanda Msangi alisema chanzo ni
madereva kupinga faini ya Sh250,000 iliyotolewa na maofisa wa Mamlaka ya
Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) kwa madereva wawili baada
ya kukiuka taratibu za usafirishaji.
Tukio
la kugoma kwa madereva hao ni la pili kwa wiki hii, la kwanza likiwa limetokea
Jumatatu ambalo lilisuluhishwa baada ya viongozi wa Sumatra kukutana na wadau
hao pamoja na polisi na kuafikiana kwamba mabasi yaliyokamatwa yaachiwe.
Mwenyekiti
wa madereva hao, Damdam Mwandubya hakuweza kupatikana, lakini dereva
aliyejitambulisha kwa jina la Geofrey Masanja alisema waligoma ili kushinikiza
mabasi yaliyopigwa faini, yaachiwe.
Maafa
Shinyanga
Mkoani
Shinyanga wachimbaji wadogo 19 walifukiwa na kifusi wakiwa ndani ya mgodi mdogo
wa Kalole kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Wachimbaji
hao walikuwa wameingia kwenye mashimo nane ambayo baadaye yalibomoka kutokana
na kufunikwa na udongo, jambo lililosababisha vifo vyao.
Mkuu
wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya alisema vijana hao waliingia katika mashimo
hayo saa 12:00 jioni kwa lengo la kuiba mawe baada ya muda wa kufanya kazi
kumalizika.
“Unajua
hawa ndugu zetu ni wale wachimbaji wasiokuwa na mashimo ambao muda ukiisha wa
kazi huingia kwenye mashimo hayo bila kuangalia usalama na ndivyo ilivyotokea
kwa wachimbaji hao,” alisema Mpesya.
Mpesya
alisema kazi ya kufukua maiti hizo lilianza, lakini lilikwama kutokana na hali
ya unyevunyevu kwenye mashimo hayo ambayo bado yanaendelea kutitia.
“Kati
ya maiti 19, saba tayari zimeshatambuliwa na ndugu zao huku nyingine mbili
zikiwa bado hazijatambuliwa na tayari tumeomba mashine ya kufukua na ya
kunyonya maji kutoka mgodi wa Bulyanhulu ili itusaidie,” alisema
Hata
hivyo, Mpesya alisema idadi hiyo inaweza kuongezeka baada ya kazi ya kufukua
kukamilika kwa kuwa hawawezi kujua kama maiti hizo 19 ndio idadi pekee ya watu
waliokuwemo ndani ya mashimo hayo.
“Tunasubiri
wenzetu kutoka mgodi wa Bulyanhulu waje waone kwanza mitambo ipi ambayo inaweza
kutumika kuyafukua mashimo hayo kwa kuwa ufukuaji wa kienyeji tuliokuwa
tukitumia tumeusimamisha kutokana na mashimo hayo kuendelea kutitia,” alisema
Mpesya.
Machimbo
hayo yaliyoko katika kijiji cha Kalole katika kata ya Lunguya Halmashauri ya
Msalala, ni moja kati ya migodi ya wachimbaji wadogo wanaokisiwa kufikia 30,000
na tayari wengi wao wamejipatia mamilioni ya pesa kwa uchimbaji huo wa kienyeji
hali ambao si salama.