Mwenyekiti wa makampuni Dr Reginald Mengi amesema anahofia usalama wa maisha yake kufuatia habari iliyoandikwa kwenye gazetimoja la kila wiki kwamba Rais Jakaya Kikwete aliapa kupambana naye Jambo ambalo limempa hofu kubwa.
Kadhalika, amelalamikia
Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu na Idara ya Habari Maelezo kwa kukaa kimya
na kuacha kutoa ufafanuzi dhidi ya tuhuma hizo, huku taarifa hizo zikiendelea
kusambazwa.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam, Mengi alisema kuwa tuhuma zilizotolewa dhidi yake
kuwa yeye ni kinara wa kuhujumu serikali ya Rais Kikwete siyo za kweli.
Dk.Mengi alisema amesoma kwa
masikitiko makubwa habari iliyochapishwa Machi 23, mwaka huu na gazeti la Taifa
Imara, yenye kichwa cha habari 'Zitto amchongea Mengi kwa JK' ambapo pamoja na
mambo mengine inasema kuwa Zitto Kabwe amemchongea Dk. Mengi kwa Rais Kikwete
kwamba ndiye kinara wa kuhujumu serikali yake.
Alisema habari hiyo ambayo chanzo
chake kimeelezwa kwamba ni Ikulu, iliendelea kueleza kuwa Zitto alikutana na
Rais Kikwete muda mfupi baada ya kuwasilisha bungeni ripoti ya Kamati ya Bunge
ya Hesabu za Serikali (PAC) kuhusiana na kashfa ya Escrow ambayo Zitto alikuwa
ni mwenyekiti wake.
"Habari hiyo inasema kwamba
katika mazungumzo yake na Rais Kikwete Zitto amenukuliwa akimueleza mkuu huyo
wa nchi kuwa anayesababisha serikali yake iyumbe kila mara ni Mengi,"
alisema Dk. Mengi.
Dk. Mengi alisema habari hiyo ambayo
nakala yake ameiambatanisha kwenye taarifa yake, inasema yeye Zitto , binafsi
amekuwa akishawishiwa na Dk. Mengi kuiangusha serikali ya Rais Kikwete.
Hata hivyo, Dk. Mengi alisema katika
habari hiyo Zitto alikwenda mbali zaidi kumueleza Rais Kikwete kuwa Dk. Mengi
ameapa kuwa Rais Kikwete akimaliza muda wake wa Urais atamshughulikia kwa nguvu
zake zote.
Alisema habari hiyo imeeleza kwamba
baada ya maelezo hayo, Rais Kikwete aliapa kupambana na Dk. Mengi na
akamshukuru Zitto kwa kumpa taarifa hizo.
Mengi alisema tuhuma zilizotolewa
kuhusu nia yake ya kutaka kuiangusha serikali ya Rais Kikwete na kumshughulikia
baada ya kumaliza muda wake wa uongozi, zimemshtua sana na tamko la kwamba Rais
Kikwete aliapa kuwa atapambana na yeye zimempa hofu kuhusu mustakabali wa
maisha yake.
Alisema kuwa hofu yake kubwa
inasababishwa na Ikulu na Idara ya habari Maelezo kukaa kimya kwa zaidi ya wiki
tatu bila kutoa ufafanuzi wowote.
"Najua umakini wa Kurugenzi ya
Mawasiliano Ikulu na Idara ya habari Maelezo katika kutoa ufafanuzi wa haraka
wa jambo lolote linalomhusu Rais, lakini katika hili nashangaa kuona taasisi
hizo zimeamua kukaa kimya na kuacha tuhuma hizo kusambaa,"alisema Dk.
Mengi.
Aliongezea kusema kuwa," hofu
yangu inazidi kuwa kubwa kwa sababu Rais ni Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na
usalama. Kauli yake kama ilivyonukuliwa na gazeti hili kwamba atapambana na
mimi inawezekana kuchukuliwa kama agizo kwa vyombo vya dola kuniangamiza,"
alisema.
Alitolea mfano mwaka 1170, Askofu
Mkuu wa Canterbury nchini Uingereza aliuawa baada ya walinzi wa mfalme kusikia
mfalme akisema "hakuna anayeweza kuniondolea huyo mkorofi?". Walinzi
wake wakadhani mfalme ameagiza wamuue Askofu huyo na wakamuua, alisema.
Chanzo NIPASHE