Wakati wapenzi na mashabiki wa Simba wakiwa wamekaa tayari kumpokea mshambuliaji wao mpya Mrundi, Laudit Mavugo, imevuja kuwa deni la milioni 20 wanalodaiwa Wekundu hao wa Msimbazi, linaweza kufuta ndoto zao za kumpata nyota huyo.
Mshambuliaji wao mpya wa Simba Mrundi, Laudit
Mavugo.
Simba wanadaiwa fedha hizo na Klabu ya Vital’O ya
Burundi zikiwa ni gharama za uhamisho wa Warundi wawili waliowahi kusajiliwa na
timu hiyo misimu miwili iliyopita ambao ni Amissi Tambwe na Gilbert Kaze.
Habari za kuaminika kutoka Vital’O ambazo Championi
Jumatano limezipata, zimedai kuwa uongozi wa klabu hiyo umeitaka Simba
ilipe kwanza fedha hizo ndipo iweze kumruhusu mchezaji huyo kujiunga na
mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Bara.
“Mavugo yupo tayari kuja kuitumikia Simba lakini
uongozi umegoma kumruhusu kujiunga na timu hiyo kutokana na kuidai klabu hiyo
kiasi cha dola 10,000 ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 20 za Kitanzania.
“Fedha hizo ni zile ambazo Simba ilitakiwa
kuzilipa wakati ilipowasajili Tambwe na Kaze misimu miwili iliyopita ambazo
mpaka sasa hazijalipwa, hivyo uongozi imebidi umzuiye Mavugo kutua Simba mpaka
hapo watakapokuwa wamelipwa deni hilo,” kilisema chanzo hicho cha kuaminika.
Hata hivyo, alipotafutwa Rais wa Simba, Evans
Aveva simu yake iliita tu bila ya kupokelewa.
Na hata alipotafutwa msemeji wa timu hiyo, Haji
Manara simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.
Kuhusiana na hilo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji
ya Simba, Collins Frisch aliyesafiri hadi Burundi kushughulikia suala la
Mavugo, alisema kweli Simba inadaiwa.
“Ni kweli, tunadaiwa dola elfu tano za zamani.
Hilo tumelikubali na tuko kwenye mchakato wa kumalizana na Vital’O. Lakini si
kweli kwamba wameweka masharti kwamba Mavugo hawezi kuja hadi hapo
tutakapowalipa.
“Kaze yeye pia aliomba Vital’O wamsaidie kutudai,
lakini rekodi zetu zinaonyesha ameshalipwa. Hivyo hatuna deni naye. Tena hata
suala la Mavugo bado hatujafikia mwafaka hivyo hawawezi kuzuia kama
ulivyosikia,” alisema Frisch.