Wakati Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim
Jecha, akimtangaza Dk. Ali Mohammed Shein, kushinda uchaguzi wa marudio
wa Machi 20, mwaka huu kwa kura 299,982 sawa na asilimia 91.4, Marekani
na Umoja wa Ulaya wameeleza kusikitishwa kwao juu ya uchaguzi huo
kufanyika bila kuwepo maelewano ya pande zinazokinzana.
Wamesema ili uweze kuaminika na kukubalika ni lazima mchakato wa
uchaguzi uwe jumuishi na unaowakilisha kwa dhati matakwa ya watu.
Wakati mabalozi hao wakisema hayo, Rais John Magufuli, amemtumia
salamu za pongezi Dk. Shein kufuatia ushindi huo akisema unaonyesha
wananchi wanataka awaongoze kwa miaka mingine mitano.
TAMKO LA MABALOZI
Tamko la pamoja lilitolewa jana na mabalozi na wawakilishi wa nchi
za Ubelgiji, Canada, Denmark, Umoja wa Ulaya, Finland, Ufaransa,
Ujerumani, Ireland, Italia, Uholanzi, Norway, Hispania, Sweden,
Switzerland, Uingereza na Marekani.
“Tumesikitishwa na uamuzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) wa
kuendesha marudio ya uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, bila
kuwepo makubaliano ya pamoja baina ya pande kinzani na ufumbuzi wa
mgogoro wa kisiasa visiwani humo uliotokana na majadilino baina ya pande
husika.
“Ili uwe wa kuaminika na kukubalika ni lazima mchakato wa uchaguzi uwe jumuishi na unaowakilisha kwa dhati matakwa ya watu.
“Tunarejea wito wetu kwa Serikali ya Tanzania kuonyesha na kuchukua
uongozi katika suala la Zanzibar na kujielekeza katika kupatikana kwa
ufumbuzi wa mgogoro huu kwa kupitia mazungumzo baina ya pande husika kwa
lengo la kudumisha amani na umoja katika Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
“Kwa mara nyingine tunawapongeza wananchi wa Zanzibar kwa utulivu
na ustahimilivu waliouonyesha katika kipindi chote cha mchakato huu na
kuvitaka vyama vyote na wafuasi wao kuanzisha tena mchakato wa
maridhiano ya kitaifa ili kupata ufumbuzi jumuishi, endelevu na wa
amani.”
Rais Magufuli
Katika salamu hizo Rais Magufuli amesema ushindiwa Dkt Shein
umedhihirisha imani na matumaini makubwa waliyonayo wazanzibari kwake na
kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwakushiriki
katika uchaguzi huo kwa amani na utulivu, na hatimaye kumpata mshindi
wa kiti cha Urais ambaye atawaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
"Naomba nikupongeze kwa dhati Mheshimiwa Rais Mteule Dk. Ali
Mohammed Shein, kwa ushindi ulioupata, ushindi ambao umeonesha kuwa
wananchiwa Zanzibar bado wanahitaji uwaongoze kwakipindi kingine cha
miaka mitano," alisema Rais Magufuli.
Pia ameahidi kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
itaendelea kufanya kazi bega kwa bega na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar
(SMZ) na amewataka Wazanzibari wote kujielekeza katika maendeleo kwa
kuwa uchaguzi umekwisha.
Chanzo: Nipashe