Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimepeleka shauri Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza kuomba ufafanuzi wa zuio la polisi kutoruhusu kuagwa kwa mwili wa aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Geita, Alphonce Mawazo.
 
Uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha pamoja jana kati ya uongozi wa Chadema chini ya aliyekuwa mgombea urais wa Chadema na kuungwa mkono na vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa; Waziri Mkuu (mstaafu), Frederick Sumaye na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe na familia ya marehemu.
 
FREEMAN MBOWE
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Mwanza, Mbowe alisema wamefikia hatua hiyo, baada ya kuona Jeshi la Polisi haliwatendei haki katika kushughulikia mazishi ya Mawazo.
 
“Tumekubaliana kuahirisha shughuli za mazishi, tunatafuta haki mahali pengine kwa kuwa hatutendewi haki na polisi, hivyo tumeamua kupeleka shauri mahakamani kuomba itoe tafsiri ya jambo hili na tunategemea Mahakama itatenda haki na kutoa tafsiri kama ni halali kwa polisi  kuzuia haki ya kuabudu na kulazimisha watu wasiage mwili wa mpendwa wao,” alisema Mbowe.
 
Alisema Chadema si chama cha kigaidi kwani kinafanya kazi zake kwa mujibu wa sheria za nchi na kwamba waliwasiliana na Inspekta Jenerali wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, wakati akiwa Dodoma na kumweleza kutoridhishwa na uamuzi huo usio wa haki wa Kamanda wa Polisi Mkoa Mwanza, Charles Mkumbo,  na Mkuu wa Wilaya ya Geita, Manzie Mangochie, kuzuia mwili wa Mawazo usiagwe.
 
Mbowe alisema iwapo mchezo huo utaachwa uendelee, ipo hatari nchi ikatumbukia katika machafuko, huku akihoji kutozuiwa mikusanyiko ya Ibada Jumapili (makanisani), misikitini, sokoni na viwanja vya michezo kwa kisingizio cha kipindupindu au ni kwa Mawazo tu.
 
 LOWASSA
Akizungumzia kadhia hiyo, Lowassa alisema polisi kama hawana kazi ya kufanya ni heri wapunguzwe, wasitafute kazi za kuwachokoza wananchi ili wayatumie mabomu na magari ya maji ya washawasha yaliyonunuliwa mengi bila sababu, bali waache wamzike ndugu yao.
 
“Uchaguzi umemalizika, maneno ya vyama yaishe na mabaya tutaendelea kuyasemea. Hivi sasa watu waliokuwa wakiunga mkono Ukawa wameanza kufuatiliwa kwa mfano, mfanyabiashara mmoja wa Mpwapwa amefungiwa shule yake…mambo haya si mazuri bali naomba viongozi waache watu waishi kwa amani. 
 
Tukiwataka wafuasi wetu wafanye wanachotaka hakutakuwa na amani,” alisema Lowassa.
 
Lowassa ambaye pia aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Nne, aliwataka polisi waache ubabe kwani nchi hii inaweza kuendeshwa bila uwapo wao, na kwamba wao ndiyo chokochoko ili watu wajaribiwe kwa  mabomu na maji ya kuwasha, hivyo wasitafute  kazi ya kuwachokoza.
 
SUMAYE
Naye Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye, alisema Tanzania ni nchi tulivu na amani, lakini mienendo inayoendelea tukifikiri tutalinda amani kwa nguvu ya dola, haki itapotea.
 
Alisema haki inapopotea amani haiwezi kulindwa kwa silaha yoyote wala nguvu ya dola, kwa kutumia silaha wala haiwezi kurejea maana huko tunakoelekea si kuzuri.
 
Sumaye alisema kuwa serikali iliukubali upinzani ambao imeanza kukua, hivyo kuukandamiza kwa nguvu ya dola ni kuleta machafuko.
 
“Mawazo kauawa, ameuawa kikatili na kifo kinachotia shaka na hakuna vurugu. Leo unapoaga mwili eti ndio vurugu zitokee, tutakuwa tunampa heshima gani. Mambo yanayotokea ni aibu na vituko vinavyoelezwa, Chadema haijawambia watu wake wachukue hatua, ni kitu cha kutengeneza ili kuchanganya juhudi hizi na Chadema watakuwa wa mwisho kuona fujo zinatokea, hatutaki watu wafike huko,” alisema Sumaye.
 
Alisema anashangazwa kusikia kuwa waombolezaji watafanya fujo, lakini wakati anauawa hilo halikutokea.
 
MLEZI WA MAREHEMU
Kwa upande wake, baba mlezi wa marehemu Mawazo, Mchungaji Charles Lugiko, alisema wanafamilia hawajatendewa haki na Jeshi la Polisi kutokana na kuwasambaratisha ndugu waliokuwa msibani nyumbani kwake Malimbe, jijini Mwanza jana.
 
Mchungaji Lugiko alisema wanasikitishwa na jeshi hilo kutumia nguvu kubwa kuzuia msiba wa Mawazo kama mtu aliyeuawa kwa tuhuma za ujambazi ama wizi, hali ambayo imewatia wasiwasi mkubwa ndugu wa familia.
 
“Mawazo aliwahi kuniambia hawezi kuvaa suti wala kuendelea na masomo ya juu, kama akifa sauti yake itaendelea kusikika Tanzania nzima, hivyo nina haki ya kumuaga na kumzika mwanangu na familia tunaungana na uongozi wa Chadema kufikisha suala hili Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, kupata ufafanuzi wa zuio la polisi ya kutomuaga mpendwa wetu, tutakubaliana na uamuzi utakaotolewa,” alisema Mchungaji Lugiko.
 
 RPC MKUMBO
Awali, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Charles Mkumbo, alisisitiza amri ya polisi ni kutoruhusu mwili huo kuagwa jijini Mwanza kutokana na sababu za kiusalama licha ya Mawazo kuwa kiongozi wa kitaifa akiwa mwenyekiti wa mkoa wa Geita (Chadema), Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Mjumbe wa Baraza Kuu na Katibu Mwenezi Kanda ya Ziwa Magharibi, ikijumuisha mikoa ya Kagera, Geita na Mwanza.
 
Mawazo aliuawa Novemba 14, mwaka huu, na watu wasiojulikana ambao hata hivyo, wanadaiwa kuwa ni wafuasi wa chama kimoja cha siasa katika kijiji cha Katoro.

 
Top