Marehemu Coster Peter enzi za uhai wake
Madai mazito! Kiongozi wa chama cha ACT - Wazalendo Kijiji cha Vitonga Kata ya Malali Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro. Coster Peter Makalius (55), anadaiwa kuuawa kikatili na mgoni wake, Mabula John, chanzo kikielezwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Tukio hilo la kuhuzunisha lilijiri hivi karibuni katika Kijiji cha Vitonga eneo la Kidai katikati ya mashamba yanayomilikiwa na Profesa wa Chuo Kikuu cha Mzumbe aliyetajwa kwa jina moja la Bujiku ambapo kigogo huyo wa ACT ndiye aliyekuwa msimamizi mkuu wa mashamba hayo.
Mwanahabari wetu alipofika eneo la tukio alishuhudia mwili wa Makalius ukiwa umelazwa kwenye majani ya migomba huku kichwa chake kikiwa kinavuja damu na ubongo baada ya kupigwa na jembe kichwani huku Mabula naye akiwa hoi kwa kipigo cha raia wenye hasira kali.
Wakihojiwa na mwandishi wetu mashuhuda wa tukio hilo, Yohana Ngana na Mogella Kibwana Mihambo walisema: “Sisi ni miongoni mwa watu tuliokodi mashamba ya Profesa Bujiku.
 Familia Ya marehemu

“Ametukodishia na tunamlipa heka moja ndoto moja (ndoto ni gunia moja la kilo 100, iwe mpunga au mahindi inategemea umelima nini) na mashamba hayo msimamizi mkuu alikuwa ni Makalius.
“Mabula alitakiwa kutoa ndoto lakini cha kushangaza aliinua jembe na kumlima kichwani Makalius.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Vitonga, Francis Anthony Kinolo alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo kijijini kwake.

Baada ya kutoka ofisi ya kata, mwandishi wetu alifka nyumbani kwa marehemu na kufanikiwa kuzungumza na mtoto wa marehemu, Evarist Makalius ambapo ndiye aliyebumburua kisa cha mkasa huo wa kusikitisha kwamba baba yake alikuwa akimtuhumu Mabula kutembea na mkewe.
“Chanzo cha kifo cha baba ni mama wa kambo ambaye alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mabula kwa siku nyingi.
Katika ugomvi wao baba anayedaiwa kutembea na mama alidaiwa kumuua baba. Ile ishu ya mashamba ni bosheni tu.
“Chanzo kikuu ni hiki cha wivu wa mapenzi,” alisema Evarist huku akiangua kilio.
Mke huyo wa marehemu, Anna Gasper alipotakiwa kuzungumzia tukio hilo alisema:

Mtuhumiwa
“Mume wangu alisema anajisikia vibaya, akanituma niende shamba nikachume nyanya, niliporudi nyumbani naye akaniaga anakwenda shamba cha ajabu baada ya muda, nilipokea taarifa kwamba Mabula amemuua mume wangu,” alisema mama huyo.

Alipoulizwa kama alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Mabula alisema anashangaa kusikia watu wakidai hivyo.
Jeshi la polisi mkoani hapa limethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba mtuhumiwa atafikishwa mahakamani wakati wowote

 
Top