Mkuu wa Wilaya ya Mpanda
Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Paza Mwamlima, ameagiza kuwa mtu yeyote atakayeugua  ugonjwa wa kipindupindu  akitibiwa na kupona, atafikishwa mahakamani kujibu kosa la kukiuka taratibu za afya na kuugua ugonjwa huo.
Mwamlima alitoa agizo hilo jana wakati wa uzinduzi wa usafi wa mazingira na upandaji miti uliofanyika eneo la Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi.
Alisema yeyote atakayeugua ugonjwa wa kipindupindu  wilayani Mpanda, atapatiwa matibabu, lakini akishapona, atashtakiwa kwa kukiuka kanuni za usafi.
Mwamlima alisema ugonjwa wa kipindupindu  huababishwa na uchafu, hivyo kama mazingira ni masafi, mtu hataugua maradhi hayo.
Aliongeza kuwa wajibu wa kila mtu kuishi kwenye mazingira safi na kuuchukia uchafu ili kuepuka magonjwa ya mlipuko.
Mkuu huyo wa Wilaya amepiga marufuku baa kufunguliwa  muda  wa kazi na kucheza  bao  na watu kushinda kwenye vijiwe  vinavyouza kahawa.
Kwa upande  wake, Mkuu wa  Mkoa wa Katavi, Dk.  Ibrahim  Msengi, amewaagiza wananchi wa manispaa hiyo kuhakikisha maeneo yao ya kuishi na wanayofanyia shughuli za biashara yanakuwa katika hali ya usafi.  Alisema kila Jumamosi wananchi wa manispaa hiyo  wahakikishe siku hiyo wanaitumia kufanya usafi kwenye mitaa yao na kwa Jumamosi ya kwanza ya mwezi, itakuwa inatumika kwa ajiri ya manispaa nzima ya Mpanda.

Chanzo: Nipashe

 
Top