Mhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, Iddi Mashaka, amekamatwa
na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika na tukio la utunguaji wa
helikopta namba 88HF na kusababisha kifo cha rubani wake, Rogers Gower,
raia wa Uingereza.
Ilielezwa kuwa Mashaka, ambaye pia ni ofisa intelijensia wa hifadhi
hiyo, anadaiwa kuwa kinara mkubwa wa ujangili katika hifadhi mbalimbali
zilizoko Kanda ya Ziwa kwa kutoa ushirikiano kwa majangili pamoja na
kuwaazimisha silaha za kufanyia uhalifu huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Simiyu, Lazaro Mambosasa, alisema Mashaka (49) ni mwajiriwa wa Hifadhi
ya Ngorongoro.
Kamanda Mambosasa alisema Jeshi la Polisi mkoani Simiyu, chinio ya
Mkuu wa Upelelezi, Jonathan Shana, liliendesha msako maalumu
uliowashirikisha askari wa vyeo mbalimbali, kikosi kazi na askari wa
wanyamapori na wananchi, hivyo kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wenzake
wanane walioshiriki katika tukio hilo.
Kamanda aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Shija Mjika, Njile Gonga,
Masasi Mandago, Mwigulu Kanga, Mapolu Njile, Dotto Huya, Mange Balum na
Dotto Pangali ambao walidaiwa kuhusika na tukio hilo la kikatili
lililokatisha maisha ya rubani wa helikopta iliyokuwa ikifanya doria
eneo la Gululu ndani ya Hifadhi ya Maswa katika kitalu cha mwekezaji,
Mwiba Holding Ltd.
Alimtaja Dotto Pangali kuwa ndiye aliyetungua ndege hiyo kwa
kutumia bunduki aina ya Rifle namba 7209460 CAR na 63229 na kwamba
alipohojiwa alikiri bunduki hiyo ni mali ya Mange Magima.
Kamanda Mambosasa alisema katika tukio hilo, Shija, Njile na Masasi
Mandago, walitoa ushirikiano wa karibu kwa kuwaonyesha meno mawili ya
tembo yenye uzito wa kilo 31 waliyokuwa wameyaficha chini ya daraja
katika kijiji cha Itaba.
Aliongeza kuwa mbali na tukio la kukamatwa watuhumiwa hao na meno
mawili ya tembo, Jeshi la Polisi lilikamata bunduki 29 na risasi 141
ambazo wamiliki wake wamekamatwa kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na
kukiuka masharti ya umiliki wa silaha.
Kamanda huyo alitoa wito kwa wananchi wote wa mkoa wa Simiyu kutoa
ushirikiano pindi wanapohisi kuna taarifa zozote za wahalifu. Pia
aliwataka kutojihusisha na vitendo vya ujangili na kuwasihi kutii.
Chanzo: Nipashe