Siku chache baada ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka kupiga
marufuku mahakama za kimila maarufu kama dagashida ambazo zimekuwa
zikihukumu watumishi wa serikali wakiwemo waalimu wa shule za msingi
kuchapwa viboko, waalimu 20 wa shule ya msingi Nkindwabiye iliyoko
wilayani Bariadi wameikimbia shule hiyo kwa kuhofia maisha yao kufuatia
kukithiri kwa vitisho wanavyofanyia kijijini hapo na wananchi.
ITV imefika katika ofisi za halmashauri ya wilaya hiyo na kuwakuta
waalimu hao ambao walikuwa na mizigo na watoto wao ambapo wamesema
wamechoka kuvumilia vitendo wanavyofanyiwa na wananchi wa kijiji hicho
ikiwa ni pamoja na kuwachomea pamba yao na kuwafyekea mazao yao ambayo
yako shambani huku wakiwaambia kuwa iwapo hawatahama mwaka huu
hawataumaliza.
Akizungumza kwa niaba ya katibu wa chama cha waalimu wilaya ya
Bariadi, Mwalimu Joyce Maisa amesema wao kama chama cha waalimu hawako
tayari kuona walimu wanapata madhara ambapo ameuomba uongozi wa wilaya
kuifunga shule hiyo hadi hapo jamii ya kijiji hicho itakapoona umuhimu
wa shule yao kuwa na walimu.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya hiyo Ponsiano Nyami amekiri kupokea
malalamiko ya waalimu hao ambapo kesho ameahidi kufika kijijini hapo kwa
ajili ya kuongea na wananchi wa kijiji hicho ili kujua hatima ya suala
hilo.
Uchunguzi uliofanywa na ITV mkoani hapa umebaini kuwa baadhi ya
wanasiasa wakiwemo madiwani wamekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha
mahakama hizo za kimila zinafanya kazi ambapo zimekuwa hazifuati sheria
za nchi na badala yake zimekuwa zikitoa maamuzi yasiyo sahihi hali
ambayo iwapo haitaisha upo uwezekano wa watumishi wengi hususani
waalimu, kuukimbia mkoa wa Simiyu.