Mwenyekiti
na Afisa mtendaji wa kijiji cha Mkwajuni wilayani Songwe, wanashikiliwa
na jeshi la polisi, baada ya wananchi kuwatuhumu kwa kutafuna zaidi ya
shilingi milioni 12 mali ya kijiji hicho pamoja na kushindwa kusoma
mapato na matumizi ya kijiji kwa zaidi ya miezi tisa.
Wananchi walionyesha furaha yao, wakishangilia hatua ya viongozi
wao kupelekwa mahabusu baada ya kufanyika mkutano wa hadhara ambao
wananchi hao waliutumia kuazimia viongozi hao wakamatwe kwa tuhuma za
kufanya ufisadi wa zaidi ya shilingi milioni 12 za ushuru wa minara ya
simu iliyopo kijijini hapo.
Wakiijitetea kwenye mkutano huo, Afisa mtendaji wa kijiji hicho
Severio Malyagila amezikana tuhuma hizo, kwa madai kuwa fedha hizo
zilitumika kwa idhini ya halmashauri ya kijiji
Hata hivyo wananchi hao hawakuridhishwa na maelezo ya Afisa
mtendaji, na baada ya mjadala mrefu ndipo mwenyekiti wa muda wa mkutano
huo, akatoa azimio kwa niaba ya wananchi, maazimio ambayo jeshi la
polisi likaanza kuyatekeleza papo hapo kwa kuwakamata watuhumiwa.