MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemhukumu kifungo cha miaka 425,
aliyekuwa Mhasibu Mwandamizi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco),
Lilian Chengula (42) baada ya kupatikana na hatia ya makosa 85 likiwemo
la kusababisha hasara ya Sh bilioni 1.3.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi alisema
mshtakiwa amepatikana na hatia ya makosa 85 kati 167 yaliyokuwa
yanamkabili na katika kila kosa atatumikia kifungo cha miaka mitano
jela.
Hata hivyo alisema, Chengula atatumikia adhabu hiyo kwa wakati mmoja
ambayo itakuwa ni sawa na kifungo cha miaka mitano jela. Akisoma hukumu
hiyo, Hakimu Shahidi alisema mshtakiwa akimaliza kutumikia kifungo
chake, atatakiwa kulipa zaidi ya shilingi bilioni moja.
Aidha aliwaachia huru washtakiwa wenzake watatu, ambao ni
mfanyabiashara Salha Salim Saad (57), Salum Saad Ally (65) na Bakary
Kinyogoli (65). Alisema anawaachia huru washtakiwa hao kwa kuwa
hawajatiwa hatiani katika makosa 82 yaliyokuwa yakiwakabili wote wanne.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri ulikuwa na mashahidi 13 pamoja na
vielelezi ili kuthibitisha mashtaka hayo. Mshtakiwa huyo alikuwa
anakabiliwa na makosa ya matumizi mabaya ya madaraka akiwa mtumishi
katika Shirika la Tanesco, na kulisababishia shirika hilo hasara ya Sh
bilioni 1.3.
Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Chengula kupitia kwa Wakili wake
Alex Mshumbusi, aliomba Mahakama imsamehe kwa kuwa ni kosa lake la
kwanza, kesi hiyo ni ya muda mrefu pia ana watoto wanaomtegemea, na muda
mrefu hakuwepo kazini.
Hata hivyo, upande wa Jamhuri uliiomba Mahakama itoe adhabu kali kwa
mshtakiwa ili iwe fundisho kwa wengine. Aidha waliiomba Mahakama itoe
amri kwa mshtakiwa huyo kulipa kiasi hicho cha fedha alichosababisha
hasara ili kulifidia shirika hilo.