MKAZI wa kitongoji cha Nyabirama kijiji cha Matongo Nyamongo, Tarafa
ya Ingwe, wilayani Tarime mkoani Mara Wambura Mrimi (50) amepata kipigo
kutoka kwa wananchi na kulazwa akiwa na hali mbaya kwa tuhuma za
kumchinja kwa kumkata shingo mke wake Maria Maningo (38) na kuchoma
nyumba zake mbili baada ya kumhusisha mke wake na imani za kishirikina.
Mrimi amelazwa katika Hospitali ya wilaya Tarime akiwa chini ya
ulinzi mkali. Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, ACP Andrew Satta alisema
kuwa tukio hilo la mauaji lilifanyika June 8, mwaka huu katika kitongoji
cha Nyabirama, kijiji cha Matongo Nyamongo baada ya kutokea ugomvi kati
ya mke na mume.
Alisema Mrimi alikuwa akimtuhumu mke wake Maria kuwa anamloga na
kushiriki katika mambo ya kishirikina lakini mke alikuwa akikana tuhuma
hizo. Kamanda Satta alisema wakati wakigombana mtuhumiwa Mrimi alikuwa
na panga mkononi ndipo alipomkata shingo mkewe na kuacha panga
limeninginia na kisha kuchoma nyumba zao mbili zilizokuwa zimeezekwa kwa
nyasi.
Thamani ya nyumba hizo na mali zilizoteketea hazikuweza kufahamika
mara moja. Alisema wananchi ambao ni wakazi wa kitongoji hicho cha
Nyabirama walisikitishwa na kitendo hicho na kuamua kupiga yowe na
kumkamata mtuhumiwa na kuanza kumshambulia kwa mawe hadi alipookolewa na
polisi waliofika mapema eneo hilo na kumchukua kwa gari akiwa
hajitambui.
Kamanda Sitta alisema mtuhumiwa huyo alikimbizwa hospitalini hapo kwa
matibabu zaidi na yupo chini ya ulinzi wa Polisi hadi sasa na mwili wa
marehemu umehifadhiwa katika Kituo cha Afya Nyamongo kwa uchunguzi zaidi
wakati ukisubiri kukabidhiwa kwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya maziko.