Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro
KIJANA aliyelelewa na nyani kwa takribani miaka nane baada ya
kuzaliwa na kutupwa porini mkoani Shinyanga na kuokolewa katikati ya
miaka ya 2000, Baraka Joshua amefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya
Ilala, akikabiliwa na mashitaka ya kulawiti na kubaka.
Joshua maarufu kama mtoto wa nyani, alipandishwa kizimbani mbele ya
Hakimu Mkazi Catherine Kiyoja. Akisomewa mashitaka hayo na Wakili wa
Serikali Florida Wenceslaus, alidai Mei 17, mwaka huu eneo la Shule ya
Msingi Tabata Kimanga, wilayani Ilala mshtakiwa alimlawiti mtoto mwenye
umri wa miaka tisa (jina linahifadhiwa).
Wenceslaus alidai katika mashitaka ya pili, siku hiyo mshitakiwa
alimbaka mtoto huyo ambaye alikuwa anasoma katika shule ya msingi
Kimanga. Mshtakiwa alikana mashitaka yote na kwamba amerudishwa rumande
baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.
Hakimu Kioja aliyataja masharti ya kuwa awe na wadhamini wawili kati
yao mmoja awe mtumishi wa Serikali watakaotia saini ya Sh milioni mbili
kila mdhamini, kesi itatajwa Mei 26, mwaka huu. Inaelezwa kuwa awali
mshtakiwa alikuwa anaishi na nyani kabla hajachukuliwa na watu wa
Maliasili baada ya kumfuatilia kwa karibu.
Ilidaiwa mshitakiwa alipochukuliwa na watu hao alifikishwa katika
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) na kuanza kutibiwa kwa kufundishwa
namna ya kutembea. Mshtakiwa alikuwa amezoea maisha ya nyani, kwani
alikuwa anatembea kama nyani na kuongea sauti ya nyani.
Baada ya kutibiwa alitokea msamaria mmoja ambaye alikuwa anaishi naye
na aliamua kumpa Joshua biashara ndogo ya kufanya katika shule ya
msingi Kimanga ambapo inadaiwa ndiko alikombaka mtoto huyo.