WANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha St Joseph (SJUIT) Kampasi ya Arusha
(kilichofutiwa usajili), waliokuwa chini ya programu ya shahada ya miaka
mitano ya ualimu wa sayansi, wametakiwa kusoma ngazi ya cheti au
stashahada. Kama watataka kusoma ngazi ya juu, watapaswa kuomba upya
udahili.
Aidha, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi
imesema wanafunzi waliokuwa wakipata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), mikopo yao pia imesimamishwa.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya
Ufundi, Profesa Simon Msanjila alitoa agizo hilo jana kupitia taaarifa
kwa vyombo vya habari. Profesa Msanjila alisema hatua hiyo, inatokana na
kubainika kwamba wanafunzi hao hawastahili kusoma shahada na pia
hawakustahili kupewa mkopo.
“Tunawafahamisha wanafunzi wa SJUIT waliokuwa kwenye programu ya
miaka mitano kwamba watatakiwa kuishia daraja la cheti na stashahada...
Kama wanafunzi hao watataka kuendelea na masomo ya juu, watatakiwa
kuomba upya,” ilisema taarifa hiyo.
Februari 25, mwaka huu, Wizara kupitia Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) baada
ya kujiridhisha kuwa Kampasi ya Arusha ya Chuo Kikuu cha Mt. Joseph
Tanzania imepoteza sifa na vigezo vya kuendelea kutoa elimu ya chuo
kikuu, ilifuta kibali cha kuanzishwa kwake.
Iliidhinisha uhamisho wa wanafunzi wote, waliokuwa wanasoma katika
Kampasi hiyo ya Arusha kwa gharama za Chuo Kikuu cha SJUIT. Aidha,
ilifuta udahili wa wanafunzi wapya katika programu ya shahada ya miaka
mitano ya ualimu wa sayansi.
Ilielekeza wanafunzi waliokuwa wakiendelea na masomo katika programu
hiyo, wahamishiwe katika Kampasi ya Luguruni, Dar es Salaam. TCU
ilielekeza kwamba wanafunzi watalazimika kwanza kuhitimu katika ngazi ya
Stashada, kama ilivyokuwa imeidhinishwa na Tume hapo awali. Wanafunzi
waliohamishiwa kwenye vyuo mbalimbali, waendelee na masomo.
Taarifa hiyo ilisema wakati wa mchakato wa uhamisho, wanafunzi wote
walihakikiwa kubaini kama wanakidhi vigezo vya kusoma kwenye ngazi hiyo.
Wanafunzi wote waliokuwa wakisoma programu hiyo ya miaka mitano,
walihamishiwa kwenye Kampasi ya Luguruni, jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo kutokana na mchakato wa uhakiki, baadhi ya wanafunzi
walikutwa hawana sifa za kujiunga na mafunzo hayo ya ualimu. Wale
waliobainika kuwa na sifa, walitaarifiwa kuendelea na masomo kwenye
kampasi hiyo ya Luguruni.
Wanafunzi katika kundi hili waliobainika kuwa na vigezo,
walitaarifiwa kuendelea na masomo katika Kampasi ya Luguruni. Maana ya
kuwa na vigezo vya ufaulu tunavyovizungumzia hapa ni kwamba wanafunzi
husika wamefaulu katika masomo lengwa yanayowawezesha kusoma Cheti cha
Ualimu Daraja “A” ambacho ni kigezo cha kwanza kwa mujibu wa mtaala wa
programu hiyo.
Chanzo: HabariLeo