ASKARI mgambo, Stinus Shirangazi (40), amepigwa na kutobolewa jicho la kushoto na watu wasiojulikana akiwa lindoni katika Mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya.



askari mgambo wa mbozi mkoani mbeya wakila kiapo baada ya kumaliza mafunzo


Tukio hilo limetokea juzi saa 6:00 usiku, jirani na mahala ambako mkesha wa Mwenge wa Uhuru ulikuwa ukifanyika.
Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki, Mganga Mkuu wa Zahanati ya Kiwira, Ruth Mgoda, alisema usiku wa kuamkia Juni 25, mwaka huu, majira ya saa 6:00 usiku mgambo huyo aligonga mlango wake akitaka huduma ya kwanza baada ya kuvamiwa na watu wasiojulikana.
Alisema baada ya kumhoji, alisema akiwa lindoni alifika kijana mmoja akiwa na mwanamke wakitaka waingie ndani ya mahakama kwa ajili ya kufanya tendo la ndoa lakini aliwakatalia na kuwaeleza pale ni mahala patakatifu.
Alisema baada ya kumzua, kijana huyo alimpiga na kitu chenye ncha kali jichoni na shavuni na kupelekea maumivu makali, huku jicho likitoa damu nyingi.
Mgoda alisema akiwa na muuguzi mwenzake, Leah Mgale, walimpatia huduma ya kwanza mgambo huyo na kisha kuomba usafiri pomoja na mgambo wa kata kwa ajili ya kumpeleka polisi ili apatiwe fomu ya P/3 na kumpeleka hospitali ya wilaya.
Alisema kabla ya tukio hilo, alisikia kelele za wanawake waliokuwa wakibakwa vichakani karibu na uwanja huo ambao walikuwa wakiomba msaada baada ya kundi la vijana kuendesha uhalifu huo.
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Kiwira, Ayubu Sherimo, alisema baada ya kupewa taarifa na wauguzi hao alienda hospitalini hapo asubuhi na kuambiwa kuwa amepelekwa hospitali ya mkoa ambako nako alihamishia hospitali ya rufaa.
Alisema alipofika hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya alimkuta mgambo huyo amelazwa akiwa hoi.
Ofisa mtendaji wa kata hiyo, Joseph Mwalyambwile, amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema kuwa wametoa taarifa polisi ili uchunguzi ufanyike na kuwatia hatiani wahusika.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahir Kidavashari, alisema hajapata taarifa juu ya tukio hilo na kwamba analifuatilia ili kujua namna ya kuwapata waalifu waweze kupelekwa mahakamani.