Waandamanaji wamevamia kituo kimoja
cha polisi kinachohusishwa na utekaji na kisha mauaji ya wakili mmoja
mteja wake na dereva wa teksi katika kisa kilichotikisa idara ya
sheria nchini Kenya.
Waandamanaji walioitikia mwito wa chama cha
wanasheria nchini Kenya cha kususia vikao vyote vya mahaka hadi wale
waliotekeleza unyama huo wafikishwe kizimbani, walifika kwenye kituo
hicho cha Syokimau viungani mwa mji wa Nairobi na kuvamia chumba
kinachodaiwa kutumika kuwatesa watatu hao kabla yao kukutana na mauti.
Walikiwasha
moto licha ya ulinzi mkali wa polisi waliokuwa wameshika zamu kituoni
humo ishara ya hasira inayochemka nchini Kenya dhidi ya mauaji ya watatu
hao mikononi mwa walinda usalama.
Inadaiwa walizuiliwa kwa muda katika kituo cha polisi wa utawala cha Syokimau.
Miili
yao ilipatikana katika mto wa Ol Donyo Sabuk, jimbo la Machakos,
mashariki mwa jiji la Nairobi, ikiwa imefungwa mkono na ikionekana kuwa
na ishara za majeraha.
Baadhi ya mashirika ya kutetea haki za
kibinadamu wanataka mkuu wa Polisi Joseph Boinnet na waziri wa usalama
Joseph Nkaissery wajiuzulu.
Kwa mujibu wa shirika lisilo la
kiserikali linalofuatilia visa vya ukatili wa polisi dhidi ya raia Kenya
la IMLU, mwaka 2015 watu 125 waliuawa kiholela na maafisa wa polisi.
Maafisa wanne wanaoshukiwa kutekeleza unyama huo Fredrick Leliman,
Stephen Chebulet, Silvia Wanjiku na Leornard Maina wamefikishwa
mahakamani na kuwekwa rumande majuma mawili ilikufanikisha uchunguzi.
Uchunguzi wa maiti yao umebaini kuwa walipigwa kikatili na silaha butu kichwani kabla ya kunyongwa.