kiomoni-Kibamba
WATUMISHI wawili wa kituo cha afya Lyabukande katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga wamesimamishwa kazi kwa uzembe uliojitokeza baada ya mjamzito kujifungulia kwenye varanda hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake hivi karibuni, aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo ambaye amehamishiwa jijini Mwanza, Kiomoni Kibamba alisema baada ya kupata taarifa hizo waliunda tume ya kwenda kuchunguza na kubaini uzembe ndiyo ulisababisha mjamzito kujifungua kwenye varanda.
Kibamba alisema hivi sasa wamewasimamisha kazi na kuwafungulia mashitaka ya kimaadili ya utumishi na kuwapa siku 14 kwa utaratibu wa ajira ya utumishi.
Aliwataja watumishi hao ambao ni Muuguzi Msaidizi, Zufa Musa na Peter Mazengo wa kitengo cha maabara kuwa ndio walikuwa zamu siku hiyo na kwamba walishindwa kumsaidia mzazi kitendo kilichobainika ni cha makusudi na uzembe.
“Nilikwisha tamka siku nyingi awamu hii ya tano ni awamu nyepesi kwa kufanya kazi sababu imenyooka na iko wazi na mtu akienda kinyume anatakiwa kupisha ili wabaki wanaotekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria, kanuni na katiba ya nchi kwa kuwatumikia wananchi,” alisema Kibamba.
Hata hivyo, kamati iliyoteuliwa ikiongozwa na mganga mkuu wa wilaya, Dk Athuman Pembe ilieleza kuwa baada ya mzazi kujifungua, watumishi hao walipata taarifa na kwenda kumhudumia yeye na mtoto akiwa na afya nzuri mwenye uzito wa kilo tatu na baada ya muda aliruhusiwa kurudi nyumbani.
Diwani wa Kata ya Lyabukande, Joseph Misiri, alisema aliyejifungulia nje katika varanda la kituo hicho ni Magreth Charles (22) aliyefika kituoni hapo akiwa ameongozana na mama mkwe.
Inadaiwa baada ya kufika kituoni hapo saa 7:00 mchana, walielezwa hakuna huduma na siku hiyo walishauriwa waende hospitali zingine kabla ya saa 9.30 alasiri kujifungua.
Mtendaji wa kata ya Lyabukande, Julius Lugende alisema kuwa kituo hicho kimekuwa kikilalamikiwa na wananchi kwa kile kinachodaiwa baadhi ya watumishi wake hawahudumii vizuri.