Meja-Jenerali-Projest-Rwegasira
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira, amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Frank Msaki kwa makosa ya kufanya malipo hewa ya posho ya chakula kwa watu wasio askari.
Taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali cha Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari, imeeleza kuwa Msaki amesimamishwa kazi kwa kufanya malipo hayo yanayofikia Sh milioni 305.
Malipo hayo kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni ya kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 hadi 2015/2016.
Meja Jenerali Rwegasira amesema kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu za Kijeshi, anayetakiwa kulipwa posho ya chakula ni askari peke yake na si mtu mwingine yeyote yule.
Alisema amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu huyo tangu jana, ili kupisha uchunguzi ufanyike juu ya tuhuma zinazomkabili.
Katibu Mkuu huyo amesema baada ya jalada la uchunguzi kufunguliwa na Ukaguzi Maalumu kufanywa na Mkaguzi wa Ndani wa Jeshi la Polisi, imebainika kuwa mbinu mbalimbali zimetumika ili kufanikisha malipo hayo hewa.
Kusimamishwa kazi kwa kigogo huyo, kumeonekana kuwa sehemu ya hatua za kurejesha nidhamu katika utumishi wa umma, ambapo mpaka mwanzoni mwa mwaka huu, Serikali ya Awamu ya Tano, ilikuwa imeshasimamisha kazi watumishi zaidi ya 150 kutokana na tuhuma mbalimbali.
Miongoni mwa tuhuma hizo ni pamoja na ukiukwaji wa Sheria ya Manunuzi, kutoridhishwa kwa utendaji, wizi katika taasisi za umma, ubadhirifu wa fedha za umma, utovu wa nidhamu na utumishi hewa.
 
Top