Watu wanne wamefariki dunia na wengine 27 kujeruhiwa baada ya lori moja lililokuwa limebeba Saruji kufeli breki kwenye mtelemko mkali wa mlima mbalizi na kupoteza mwelekeo kisha kuparamia magari mengine manne na watembea kwa miguu kabla ya kupinduka katikati ya mji mdogo wa mbalizi mkoani Mbeya.

Ajali hiyo ambayo imehusisha lori lenye namba za usajili T 215 CLB likiwa na tela lenye namba za usajili T 876 CLB imetokea majira ya saa mbili usiku,baada ya gari hilo kudaiwa kufeli breki likiwa kwenye mtelemko mkali wa mlima mbalizi.

Utingo wa lori hilo, Wilbaert Joseph ambaye ni mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo amesema kuwa gari lao lilimshinda dereva baada ya kukatika breki wakiwa kwenye mtelemko mkali, hali ambayo imesababisha wapate ajali.

Muuguzi mkuu wa hospitali teule ya Ifisi Erimat Sanga, amethibitisha kupokea majeruhi 22 na maiti tatu, huku muuguzi wa zamu katika hospitali ya rufaa mbeya, Lucy Elias akithibitisha kupokea majeruhi 10, kati yao watano ni wale waliopewa rufaa kutoka hospitali ya Ifisi na watano wengine kutoka eneo la ajali na kwamba majeruhi mmoja amepoteza maisha.

Kamanda wa polisi mkoa wa mbeya, Zahir Athuman Kidavashari amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
 
Top