Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limemkamata Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) alipowasili akitokea Japan.

Baada ya Askofu Gwajima kukamatwa na Kikosi cha Polisi cha Uwanja wa JNIA alipelekwa moja kwa moja Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya mahojiano akidaiwa alitoa maneno ya uchochezi mwezi uliopita.

Kamanda wa Polisi Uwanja wa JNIA, Martin Otieno amesema askofu huyo amekamatwa i akitokea Japan kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege la Kenya.

Otieno amesema amepelekwa katika Kituo Kikuu cha Polisi kwa ajili ya kuhojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

“Ni kweli tumemkamata Askofu Gwajima hapa uwanja wa ndege wa JNIA baada ya kuwasili kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya na tulipomuhoji amedai kuwa alikuwa nchini Japan,” amesema Otieno.

Mwanasheria wake Peter Kibatala amesema Gwajima amefika Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano mafupi na ameruhusiwa kuondoka baada ya kujidhamini yeye mwenyewe.

“Askofu Gwajima amehojiwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu na amejidhamini yeye mwenyewe, ameruhusiwa kuondoka hivyo tunasubiri chochote kitakachoendelea,” amesema Kibatala ingawa hakufafanua kuhusu mahojiano hayo.

Askofu Gwajima alikuwa anatafutwa na polisi tangu mwezi uliopita baada ya kusambazwa mkanda kwenye mitandao ya kijamii unaodhaniwa una sauti yake akipendekeza Rais mstaafu Jakaya Kikwete kufikishwa mahakamani kwa yote yaliyofanyika wakati wa utawala wake ambayo sasa Rais John Magufuli anayashughulikia kwa mtindo wa kutumbua majipu.

Katika mkanda huo, sauti hiyo inadai kuwa baadhi ya viongozi wa CCM wametuma watu mikoani kupiga kampeni ya kutaka Rais Magufuli asipewe uongozi wa chama hicho kwa sasa kama ilivyo utaratibu wa chama hicho na kwamba hilo likifanyika basi Rais abadili katiba ili mstaafu huyo aweze kufikishwa kortini.

Tangu ulipotolewa mkanda huo, makachero wa polisi wamekuwa wakipiga kambi nyumbani kwa Askofu Gwajima kwa lengo la kumkamata lakini hawakumpata. Baadaye ilikuja kufahamika kwamba askofu huyo alikuwa amekwenda nje ya nchi lakini haikujulikana ni nchi gani.

 
Top