DUNIANI kuna mambo, ndivyo unaweza kusema kutokana na mkazi wa Mtaa
wa Mateka, Manispaa ya Songea, Denis Komba (26) kufa baada ya nyoka wake
aliyekuwa amembeba kwenye mfuko wa jaketi kuuawa na wananchi.
Komba alifariki dunia katika hospitali ya Rufaa Songea mkoa wa Ruvuma
(Homso) ambako alilazwa baada ya watu wenye hasira kumuua kwa mawe na
fimbo nyoka wake huyo.
Mashuhuda wanaeleza kuwa kabla ya wananchi kumuua nyoka huyo, Komba
aliwasihi wasifanye hivyo kwa kuwa wakimuua na yeye angekufa, lakini
ombi lake hilo halikusikilizwa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, siku ya tukio Komba alikodi
pikipiki ya Kassian Haule (24) ambaye ni mkazi wa Mpitimbi, yenye namba
za usajili MC 724 AKB ili apelekwe nyumbani kwake mtaa wa Mateka.
Akisimulia tukio hilo, alisema alipofika katika eneo la Benki ya
Posta ya zamani barabara kuu ya Sokoine, dereva wa pikipiki alihisi kuna
kitu kinamtekenya na kumgonga gonga kwa nyuma, ndipo alipogeuka nyuma
na kumwona abiria wake amebeba nyoka mkubwa huku amesimamisha kichwa.
Haule alisema, baada ya kumuona nyoka huyo aliruka kutoka kwenye
pikipiki na kuanguka pembeni mwa barabara na abiria wake alimwachia yule
nyoka ambaye alikimbilia kwenye kalavati la maji.
Aliongeza kuwa ndipo alipopiga kelele za kuomba msaada na kundi la
vijana waendesha pikipiki wenzake walifika eneo hilo la tukio kwa lengo
la kumsaidia mwenzao juu ya maswahiba yaliyompata hadi kumfanya apige
kelele.
Alisema kabla ya vijana hao hawajafanya jambo lolote, Komba aliwaomba
vijana hao na watu wengine waliofika katika eneo hilo wasimpige nyoka
wake kwani iwapo watampiga na kufa yeye pia atapoteza maisha. Kutokana
na maneno hayo, Haule alimtoa nyoka huyo ndani ya kalavati na kwa
kushirikiana na vijana wenzake walianza kumpiga nyoka huyo hadi kufa.
Alisema wakati wanampiga nyoka huyo, Komba ambaye ndiye mmiliki wa
nyoka huyo naye alianza kulegea kisha akaanguka chini huku akitokwa na
mapovu mdomoni na puani.
Habari zinasema kuwa,baada ya Komba kuanguka alikimbizwa hospitali
kwa ajili ya kupatiwa matibabu; hata hivyo juhudi za madaktari na
wauguzi wa hospitali za kuokoa maisha yake zilishindikana kwani Komba
alifariki.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa mwili wa marehemu haukuwa na
jeraha lolote na umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti katika
hospitali ya rufaa Songea.
Alisema nyoka aliyeuawa na wananchi amechukuliwa na idara ya
maliasili na uchunguzi zaidi ya tukio hilo unaendelea ili kubaini kiini
cha tukio hilo la kuuawa kwa nyoka na kisha mmiliki wake naye kufa.
Kamanda Mwombeji alisema, kwa upande wa dereva wa pikipiki yeye
anaendelea vizuri na anapatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya
mkoa wa Ruvuma.
Aidha Kamanda Mwombeji, ametoa rai kwa wananchi kuacha mara moja
kumiliki nyara za serikali zinazoweza kuwaletea madhara kama vile
majeraha au vifo.
Chanzo: HabariLeo