WATU wanaoishi bila ndoa rasmi nchini Burundi, wametakiwa kuoana rasmi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu vinginevyo watakumbana na mkono wa sharia.
 Amri hiyo ya serikali imetolewa baada ya Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza, kuanzisha kampeni maalum ijulikanayo kama ‘kuifanya jamii yenye maadili’.
Msemaji wa serikali alikaririwa na vyombo vya habari nchini humo kwamba amri hiyo inalenga kupambana na ‘mafuriko ya ongezeko la watu’ ambalo moja ya sababu za uwapo wake ni ndoa zisizo rasmi.
Alisema wasichana wengine wamekuwa wakipata ujauzito wakiwa shuleni na wanaume wamekuwa wakitumia mwanya huo kuwaweka kinyumba na matokeo yake kuongezeka kwa idadi ya watu.
Msemaji wa Wizara ya mambo ya ndani ya Burundi, Terence Ntahiraja, aliliambia shirika la habari la AFP juzi kuwa ndoa hizo za kidini ambazo zimetangazwa na serikali ni hatua ya kutafuta ufumbuzi juu ya ongezeko la watu ambalo linatishia mipango ya maendeleo ya nchi.
Ntahiraja alikiita kitendo hicho kuwa ni cha kizalendo."Tunataka wananchi wa Burundi watambue kuwa kila mmoja anawajibika na maisha yake na tunataka ‘unyoofu’ ndani ya nchi,’ alisema.
"yote haya yanapaswa kufanyika katika muda uliopangwa kama alivyotangaza Rais (Nkurunziza),” aliongeza.Hata hivyo, haijaelezwa wazi ni hatua zipi za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale watakaokaidi amri hiyo ya Rais, licha ya kwamba amesema watakumbana na mkono wa sheria.
Wakati amri hiyo ikitakiwa kutekelezwa, mkulima mmoja alikaririwa na AFP kuwa viongozi wa serikali za mitaa wamemtishia yeye na mwenzi wake kuwa watamtoza faini na kwamba mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa atakosa nafasi ya kupata elimu na matibabu bure.
Mkulima huyo, aliyetajwa kwa jina la Pierre, alisema hakuoa rasmi kwa kuwa alishindwa kulipa mahari aliyopangiwa na wazazi wa mwenzi wake.


    TANGAZO 
 
Top