Vijana waliokuwa wameshika mapanga na marungu walifanya kazi ya kuvamia makazi ya watu na kuwateketeza kwa moto kwa kile kinachodaiwa kuwa ni imani za kishirikina.
KIGOMA: Watu 7 wameuawa katika kijiji cha Murufiti, Kasulu mkoani Kigoma majira ya saa 4:00 usiku wa terehe 6 katika mashambulizi yaliyofanywa na vijana wa kijiji hicho ambacho walivamia baadhi ya nyumba na kuzichoma moto huku nyingine kuzibomoa.
Kwa mujibu wa chanzo cha Habari hii kimeeleza kuwa, Vijana wa kijiji cha Kafuru walitembelea nyumba za watu waliosadikiwa kuwa ni wachawi huku wakiwa na silaha mbalimbali za jadi kama vile marungu, fimbo na mapanga.
Katika mashambulizi hayo jumla ya nyumba 18 ziliunguzwa moto na nyingine 2 kubomolewa na kufikisha jumla ya nyumba 20 zilizoharibiwa.
“Niliporudi alfajiri niliukuta
mwili wa mama ukiwa umbali wa mita 10 kutoka ilipo nyumba yetu ukiwa umeungua
na mwili wa baba ukiwa umeungua ndani ya nyumba,” alisema John, Kijana ambaye alifanikiwa Kutoroka usiku nyumba yao ilipovamiwa na vijana hao.
John alieleza kuwa mauaji hayo yamefanyika baada ya Mganga wa kienyeji kupiga ramli na kuwataja waliouawa kuwa ni wachawi kijijini hapo.
Watu ambao wametajwa kuuawa katika tukio hilo
John Muvumba (68), Elizabeth Kaje (55), Dyaba Kitwe (55), Vincent Ntiyaba (42),
Herman Ndabiloye (78), Redempta Mdogo (60) na Ramadhan Kalaliza (70) wote
wakazi wa kijiji hicho.
Polisi wameeleza kuwa, tayari watu 17 wamekamatwa kwa kuhusishwa na vurugu hizo. Vilevile wanaume wengi wametoroka katika makazi yao kwa kuhofia kukamatwa na polisi, na wengine kuhofia kuuawa kwa tuhuma za ushirikina.
Chanzo: Mwananchi