Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini (CDF), Jenerali Davis
Mwamunyange
Hali ya kushangaza imewakumba wananchi wa Tarime baada ya kushuhudia mapambano makali ya kurushiana risasi na kutwangana mangumi yaliyotokea kati ya askari wa jeshi la polisi na Askari wa Jeshi la wananchi Tanzania (JWTZ)
Mara: Watu 12 mkoani Mara wilayani Tarime wamejeruhiwa katika mapambano kati ya Askari wa Jeshi la wananchi (JWTZ) kikosi 128 cha Nyandoto na Polisi wa kituo cha Stendi wilayani humo.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari hii, Vurugu hizo zilizotokea Juzi majira ya saa 12 jioni baada ya Mwanajeshi mmoja kukamatwa na askari wa usalama barabarani kwa kosa la kuendesha pikipiki bila kuvaa kofia ngumu (helment)
Baada ya askari huyo kutiwa hatiani na kutakiwa kuripoti katika kituo cha polisi aligoma na kutoa lugha chafu jambo ambalo liliwafanya askari wa jeshi la polisi kumkamata kwa nguvu.
Askari wa jeshi la wananchi (JWTZ) walifika kituoni hapo na kuanzisha vurugu wakitaka mwanajeshi mwenzao aachiwe huru. Vuta nikuvute hiyo iliyotokea kati ya pande hizo mbili ilisababisha kushikana na kutwangana mangumi pamoja na kurushiana risasi za moto.
Dk. Makonyo aliwataja waliojeruhiwa kuwa ni Aloyce Filbert (24) aliyepigwa
risasi mguu wa kulia, Deodatus Dominic (26) aliyejeruhiwa puani na wote ni
askari wa JWTZ.
Wengine ni askari polisi saba ambao ni Makoye Katula (26), Sylvester Michael
(31), Salum Omary (44), Abdallah Halifa (24), Joel Msabila (25), Ally Juma (27)
na Deogratius Tryphon (32) na raia Hamza Jumanne (33) aliyepigwa risasi mguu wa
kushoto ambaye alipelekwa Hospitali ya Shitari, Rorya kwa matibabu.
Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Ndalama Salumu anadaiwa
kujeruhiwa kwa kupigwa katika vurumai hizo huku mwananchi mwingine, David
Kisaro (20) akijeruhiwa kwa bomu jichoni. Alitibiwa katika Zahanati ya Tarime.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya, Benedict Mambosasa alisema wanajeshi
watatu ambao hawakutajwa majina, wamekamatwa na polisi kwa kuvunja utaratibu wa
usalama.