MKAZI
wa kitongoji cha Ng’anandi kijiji cha Mpinga Kata ya Kigwe wilayani Bahi,
Jumanne Ichirile (23) ameua mama mkwe wake na mtoto wake mwenye umri wa miaka
miwili kwa kuwachoma visu.
Pia
amemjeruhi mkewe kabla ya kujiua kwa kujichoma na kisu tumboni, kutokana na
wivu wa kimapenzi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema tukio
hilo ni la Jumamosi iliyopita.
Waliouawa
walitajwa kuwa ni Sarah Mango wa miaka kati ya 60 na 70 na mtoto, Amina Jumanne
mwenye umri wa miaka miwili, ambao waliuawa kwa kuchomwa kwa visu sehemu
mbalimbali za miili yao.
Akisimulia
mkasa huo, mke wa mtu huyo ambaye alijeruhiwa katika tukio hilo, Elizabeth
Kulwa (21) , alisema akiwa nyumbani kwa mama yake mzazi Sarah Mango ilipofika
majira ya saa 11 jioni alivamiwa na mume huyo huku akiwa ameshika kisu mkononi.
Alisema
ghafla alianza kumshambulia na kumchoma kisu tumboni mara mbili na katika
sehemu mbalimbali za mwili wake.
Alisema
hii si mara ya kwanza kwa mwanaume huyo kumshambulia, kwani hata mwaka jana
alifanya hivyo kwa kumkatakata kwa mapanga yeye na mama yake.
Alisema
katika shambulio hilo walifanikiwa kuripoti kwenye vyombo vya sheria na kisha
kesi ikafunguliwa mahakamani ambapo mumewe alihukumiwa kifungo cha miezi minane
gerezani.
Hata
hivyo, mama huyo hana kumbukumbu mumewe huyo alitoka gerezani lini lakini
anachokumbuka ni miezi ya hivi karibuni.
Kwa
sasa Elizabeth amelazwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kwa matibabu kutokana na
majeraha aliyoyapata katika titi la kushoto, ubavuni, tumboni na mkononi.
SOURCE: Bongo Special