
Mtu mmoja anayesadikiwa kuwa ni mganga wa kienyeji, anadaiwa
kumbaka na kumwingilia kinyume na maumbile msichana mwenye umri wa miaka 19
aliyemsindikiza dada yake kwa mganga huyo kupata tiba.
Mganga huyo, Ali Abdulrahman Ali (45), anadaiwa kufanya kitendo
hicho Novemba 26, mwaka huu, nyumbani kwake eneo la Kwamtipura Wilaya ya Mjini
Unguja.
Mrakibu mwandamizi wa jeshi la polisi, kituo cha polisi
Mwembemadema, Haji Abdallah Haji, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema polisi inaendelea na upelelezi ambapo mtuhumiwa yupo nje
kwa dhamana na upelelezi utakapokamilika jalada lake litapelekwa kwa Mkurugenzi
wa Mashtaka ili afikishwe mahakamani.
Daktari wa kitengo cha mkono kwa mkono katika Hospitali ya
Mnazimmoja, Dk. Msafiri Marijani, ambaye alimpokea msichana huyo kwa uchunguzi,
aligundua kuwa ameingiliwa katika sehemu zote za siri.
Muathirika wa tukio hilo (jina linahifadhiwa) alisema, Novemba 26,
mwaka huu, alimsindikiza dada yake aliyekwenda kupatiwa tiba kwa mganga huyo na
walipofika mganga aliwataka walale hadi siku ya pili ndio tiba itakuwa
imekamilika.
Alisema ilipofika saa 7 usiku wakiwa wamelala, mganga huyo
alimfuata kitandani kwake na kumfanyia kitendo hicho huku akimziba mdomo asipige
kelele.
“Wakati tumelala mimi na dada chumba kimoja huku kila mtu akilala
kwenye kitanda chake, nilishtuka kumuona mtu amenikalia juu kifuani huku
akiniziba mdomo na kuniambia nikipiga kelele ataniua. Wakati huo dada alikuwa
amelala hana habari,” alisema.
Mama wa mtoto huyo alisema mganga huyo amekuwa akimpatia tiba
mtoto wake huyo mwenye matatizo ya akili.
Alisema baada ya kugundua mtoto wake amefanyiwa kitendo hicho,
mtoto wake mwingine mwenye umri wa miaka 35 ambaye pia hupatiwa tiba na mganga
huyo, alisema na yeye alikuwa anamfanyia kitendo hicho na kumwambia kuwa ndio
tiba ya maradhi yake.