Milima ya Uruguru imeendelea kuteketea kwa moto kwa takribani zaidi ya wiki moja sasa, huku jitihada za kuzima moto huo mkubwa unaozidi kusambaa katika maeneo mengi zaidi zikikwamishwa na jiografia ya maeneo hayo yenye milima mikali, mabonde na miamba.
Chanzo chetu kimeshuhudia moto huo mkubwa ukiwa umesambaakatika eneo kubwa la safu ya milima hiyo ya Uluguru, ambapo ilimtafuta mhifadhi wa Uluguru Nature Reserve iliyo chini ya wakala wa misitu, karani Sekiete, ambaye anakiri pamoja na milima hiyo kuwa salama kwa takribani miaka mitatu iliyopita bila tatizo la moto, kutokana na elimu zaidi kutolewa na mashirika mbalimbali na wakala wa misitu, hali imegeuka siku chache zilizopita baada ya kuzuka kwa moto huo unaosambaa kwa kasi kutokana na ukame na upepo mkali.

Mhifadhi huyo anasema wamebaini sababu mbalimbali kuchangia moto na ongezeko la moto katika milima hiyo, ikiwemo kuona viashiria vilivyoonekana kusababisha, ikiwemo uwindaji wa wanyama wadogowadogo waliopo maeneo hayo, uchimbaji wa kile kinachoaminika ni madini, na hata masuala ya kisiasa kwa baadhi ya viongozi kuwakataza wananchi kuzima kwa kuamini jukumu hilo ni la serikali, taasisi fulani au wakala wa misitu bila kutambua jukumu hilo ni la kila mtu.

Chanzo chetu kimefika ofisi za mkuu wa wilaya ili azungumzie jitihada za ziada zinazohitajika na kama wapo watu waliokamatwa kwa kuanzisha moto huo na kuelezwa kuwa mkuu huyo wa wilaya Muhingo Rweyemamu ndio kwanza alikuwa ameripoti ofisini, na aliyehusika kuzungumzia ni katibu tawala wa wilaya, ambaye alikataa kuzungumza lolote kwa madai hadi moto huo uzimike, huku wananchi wakizungumzia athari za moto huo na kuwalaani waliosababisha.


Milima ya Uluguru imekuwa chanzo kikubwa cha maji kwa wananchi wa mikoa ya Morogoro, Pwani na Dar es Salaam na imekuwa na viumbe hai ikiwemo wanyama na mimea na bionuwai zingine ambazo hazipatikani kwingineko duniani.
 
Top