Polisi nchini Ujerumani wameonya wazazi dhidi ya kuweka picha za watoto wao hadharani katika mtandao wa kijamii wa Facebook.
Katika
ujumbe kwenye ukurasa wao wa Facebook, polisi wa eneo la Hagen wametahadharisha
wazazi kuwa picha hizo zinaweza kunakiliwa au kubadilishwa na kutumiwa vibaya
na watu wanaovutiwa kimapenzi na watoto.
Aidha,
watoto wahusika huenda wasipendezwe na picha hizo kuwa wazi mitandaoni
watakapokomaa na kuwa watu wazima.
Wazazi
wameshauriwa kuhakikisha kuwa picha hizo, ikilazimu, zinatazamwa na marafiki
zao pekee na si kila mtu mtandaoni.
Ushauri
huo wa polisi hao umeenezwa sana mtandaoni na kuvutia hisia mseto.
Afisa
msemaji wa Polisi wa Hagen ameiambia BBC kwamba walishangazwa na jinsi ujumbe
huo wa tahadhari ulivyopokelewa.
Amesema
wanakadiria kuwa umesomwa na watu zaidi ya milioni 12.
"Tunataka
kuwaambia watumiaji wote wa mitandao ya kijamii kwamba ni muhimu kuwa makini na
kila kitu wanafanya kwenye mtandao," amesema Hanki Ulrich .
"Ni
bora kufikiria mara mbili - mtandao hausahau kamwe "
Bw
Hanki ameongeza kuwa ujumbe huo haujaongozwa na matukio yoyote mapya ya kesi za
uhalifu au watu wanaovutiwa na watoto kimapenzi huko Hagen.
Picha Zilizobadilishwa
Shirika
la kujitolea linalohusika na ulinzi wa watoto NSPCC katika taarifa yao
wamesema: " Wazazi wote wanapaswa kujisikia huru na kufurahia kuchukua
picha za watoto wao na kushirikiana nao na marafiki na familia. Hata hivyo,
tunapaswa wote kuwa makini wakati wa kuziweka picha hizo mitandaoni.
"Tunajua
kwamba wahalifu wa ngono wana uwezo wa kubadilisha picha za watu wasiokuwa na
hatia, na maendeleo katika programu za kuhariri picha zimefanya hili kuwa
rahisi sana.
"
Hivyo kama wazazi watachapisha picha za watoto wao kwenye mitandao, wanapaswa
kuchukua hatua ili kuhakikisha kwamba wanachunguza hali yao ya faragha na
kuhakikisha wanaridhishwa na watu watakaotazama picha hizo."
Shirika
hilo limeongeza kuwa iwapo wazazi wana wasiwasi kuwa picha ya mtoto wao
imeanguka mikononi mwa watu wabaya, wanapaswa kuwasiliana na Internet Watch
Foundation, Child Exploitation na Online Protection Centre (Ceop) au
kuwasililiana na NSPCC kupitia numbari ya msaada ya simu ya 0808 800 5000
ambapo watapokeza usaidizi.
Chanzo: BBC