Tume ya taifa ya uchaguzi (Nec), imeahidi kutangaza matokeo ya uchaguzi wa madiwani na wabunge ndani ya saa 24 wakati yale ya Rais yatatolewa siku tatu baada ya kupiga kura.
Aidha Nec imewaagiza wasimamizi wa uchaguzi kwenye
vituo kutotangaza matokeo ya ubunge na madiwani ndani ya muda huo.
Mwenyekiti wa Nec, Jaji Damain Lubuva, aliwaambia
wanahabari jana jijini Dar es Salam wakati akizungumzia upigaji kura wakati wa
uchaguzi mkuu unaofanyika leo.
Alieleza kuwa matokeo ya awali ya urais
yatatangazwa kwa hatua kadri tume itakavyokuwa inayapokea kutoka ngazi za chini.
Jaji Lubuva alisema Nec itajumlisha matokeo ya
uchaguzi wa rais wa majimbo yote kwa nchi nzima na kumtangaza mshindi.
Aidha aliwaambia mawakala wa vyama vya siasa
vinavyoshiriki uchaguzi wa rais kuwa wanaruhusiwa kuwepo wakati wa kujumlisha
matokeo ya kura hizo.
“Ni Nec pekee yenye mamlaka kisheria ya kumtangaza
mshindi wa urais. Matokeo yatakayotolewa na tume ndiyo yanayoheshimiwa,”
alisisitiza.
Aliwaambia wana habari kuwa mwaka huu wapiga kura
milioni 23.25 waliandikishwa na kwamba jumla ya vituo 64,736 vitatumiwa kupiga
kura Tanzania Bara ina vituo 63,156 na Zanzibar ni vituo 1,580, kwa mujibu wa
maelezo yake.
Aidha alisema vituo vya kupigia kura vitafunguliwa
saa 1:00 asubuhi na kufungwa saa 10:00 jioni. Iwapo wakati wa kufunga kituo
wananchi watakuwa kwenye mistari lakini ambao walifika kabla ya wakati wa
kufunga kituo wataruhusiwa kupiga kura.
Alisema baada ya kufika saa 10:00 jioni
atakayefika baada ya muda huo hataruhusiwa.
Jaji Lubuva alivitaka vyama vya siasa
vinavyoshiriki katika uchaguzi kuhakikisha kwamba vinaweka mawakala katika
vituo vyote vya kupigia kura na kushiriki kujumlisha kura na kuwataka
kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
“Baada ya kupiga kura na kwa kuzingatia maadili ya
uchaguzi ya 2015 yaliyokubaliwa na vyama vyote vya siasa na kuridhiwa na
mahakama, wapiga kura wanatakiwa kuondoka vituoni na kuendelea na shughuli zao,”
alisisitiza.
Alisema Tume inawahakikishia wananchi kuwa
kutakuwa na ulinzi wa kutosha katika vituo vya kupigia kura.
“Tunatumaini kuwa amani na utulivu iliyokuwepo
hadi itaendelea kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita ili kuhakikisha
kwamba uchaguzi unafanyika kwa utulivu na amani kwa ustawi wa taifa letu,”
alisema
Wakati huo huo , Chama cha Wamiliki wa Mabasi
(Taboa) kimesitisha safari za mikoani ili kutoa nafasi kwa madereva pamoja na
makonda kupiga kura kwani ni haki yao kikatiba.
Chanzo: Nipashe
MATUKIO ZAIDI BOFYA HAPA=>