Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein
Jeshi la Polisi jana walitumia mabomu ya machozi kurejesha hali ya
amani baada ya wananchi kuanza kupigana kwa sababu za kisiasa wakati
wakisherehekea ushindi wa Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein,
katika kijiji cha Mjini Wingwi Wilaya ya Micheweni, Pemba.
Akizungumza na Nipashe, Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Micheweni,
Rashid Khalid Salim, alidai vurugu hizo zimesababishwa na wanachama wa
CCM kutoka katika kijiji cha Kwale wilayani humo.
Alisema baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) kutangaza
matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa marudio, wanachama wa CCM katika kijiji cha
Kwale, walianza kukusanyika na ngoma zao na kuanza safari ya kuingia
katika kijiji cha Mjini Wingi, sehemu ambayo ni ngome ya wanachama wa
CUF, huku wakisherehekea kwa kurusha 'vijembe' (maneno ya kejeli) na
matusi.
“Pamoja na kutakiwa kuacha matusi wakati wakisherehekea ushindi wa
Dk. Shein, waliendelea na kusababisha wenzao kupandwa na ghadhabu
kuwachemka na kuanza kupigana,” alisema Mwenyekiti huyo.
Alisema baada ya kutokea vurugu hizo, wanachama wa CCM kutoka
kijiji cha Kwale, walilazimika kukimbilia Kituo cha Polisi Micheweni.
Alisema askari walipofika eneo la tukio, walianza kupiga mabomu ya kutoa machozi na kuvunja milango ya nyumba.
Mwenyekiti huyo alisema nyumba 15 zilivunjwa milango wakati
wakiwasaka watu waliokuwa wakihusishwa na vurugu hizo ambazo zilianza
kufanyika saa 10:00 jioni na kuendelea hadi usiku juzi.
Aidha, alisema kwa mujibu wa mabaki ya milipuko, jumla ya mabomu 27
yanadaiwa kupigwa mbali na nyumba kuvunjwa milango na kusababisha watu
zaidi ya 28 kuyakimbia makazi yao katika kijiji hicho.
“Watu wanne wamekamatwa akiwamo mtoto mwenye umri wa miaka 13,
lakini wananchi wengi wamekimbia makazi yao na kukimbilia katika kisiwa
cha Kojani na Maziwang'ombe,” alisema Rashid.
Hata hivyo, alisema jambo la kushagaza polisi wameamua kuwakamata
watu waliofanyiwa fujo badala ya kuwakamata waliokuwa chanzo cha vurugu
hizo.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Hassan Nassir,
alithibitisha kutokea kwa vurugu hizo na kwamba watu watano
wanashikiliwa kwa uchunguzi wa kuhusika na tukio hilo.
Hata hivyo, alikanusha kuvunjwa milango 15 pamoja na kutumika
mabomu 27 kurejesha hali ya utulivu baada ya wananchi kuanza kupigana.
Waliokamatwa katika mkasa huo ni Kombo Khalfan Faki, Salim Hassan
Khamis, Mjawiri Faki, Khatib Dawa Juma na Assaa Bakar Ali, wakazi wa
kijiji hicho.
Kwa upande wake, Mkuu wa mkoa huo, Omar Khamis Othman, alisema hali
katika kijiji hicho imerejea kuwa ya kawaida na kuwataka wananchi
kuendelea na sherehe za kumpongeza Dk. Shein bila ya kuvunja sheria.
Alisema wananchi waliokimbia makazi yao na kukimbilia katika kisiwa
cha Kojani na Maziwang'ombe, watakuwa ndiyo waliohusika na vurugu na
kwamba raia mwema hana sababu ya kukimbia askari.