Rufiji. Jeshi la Polisi mkoani Pwani linamshikilia mmoja wa maofisa wa Tarafa wa Kibiti kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa kike mwenye miaka 12 mkazi wa kitongoji cha Kibiti kati wilayani hapa.
Akithibitisha kushikiliwa kwa Afisa tarafa huyo, Kamanda wa Polisi mkoani Pwani Bonaventure Mushongi amesema mtuhumiwa huyo anatuhumiwa kumbaka mtoto huyo mara kadhaa akiwa ofisini kwake.
"Tunamshikilia mtuhumiwa huyo kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi huyo wa kike mwenye miaka kumi na mbili mara kadhaa ofisini anayesoma darasa la sita katika shule ya msingi Kitundu wilayani Rufiji," amesema.
Amesema kutokana na tuhuma hiyo, uchunguzi zaidi unaendelea na utakapokamilika atafikishwa kizimbani kujibu tuhuma za kubaka.
Kamanda Mushongi amesema katika maelezo ya awali ya mtuhumiwa huyo alikiri kumfahamu mwanafunzi huyo na wenzake kutokana na wanafunzi hao kuwa na mazoea ya kwenda ofisini kwake kujisomea.
Amesema mtuhumiwa huyo alikuwa akimpatia mtoto huyo kati ya Sh250 na Sh1,500 kwa ajili ya kukamilisha zoezi hilo linalotajwa alilianza mwezi January mwaka huu.
Mama mzazi wa mwanafunzi huyo akizungumzia tukio hilo amesema alipata taarifa za mwanae kuwa anabakwa na afisa tarafa huyo kupitia kwa majirani zake waliokuwa wakimuona mara kwa mara mwanae akiingia katika ofisi afisa tarafa huyo.
"Jirani yangu alikuja kuniambia kuwa mwanangu mara kwa Mara amekuwa akiingia katika ofisi ya Afisa Tarafa,na hata muda huu tumemuona akiingia ofisini kwake, kauli iliyoniinua na kuamua kufuatilia kauli hiyo," amesema mama huyo.
Amesema baada ya kufika katika ofisi ya afisa Tarafa huyo,aliwatuma watoto kwenda kumwita,lakini ghafla Afisa Tarafa alitoka nje na kuwajibu kuwa binti huyo hayupo huku akiwa anatapatapa.
Amesema baada ya muda mfupi kurudi nyumbani kwake, binti Yake alirejea na baada ya kumhoji alikiri alikuwa katika ofisi ya Afisa Tarafa huyo.
Mama huyo amesema,baada ya muda mfupi walimuomba jirani yao amhoji mtoto huyo,na ndipo alipowaeleza kwa muda mrefu kuanzia January mwaka huu amekuwa akiitwa ofisini kwake na kuanza kumtomasa tomasa kisha kuingiliwa na Afisa Tarafa huyo huku akipewa pesa kwa ajili ya matumizi ya shuleni.
"Baada ya kumhoji amesema alikuwa anamuita ofisini kwake na kumtomasa tomasa kisha kumuingilia na kumpatia kati ya shilingi mia mbili na hamsini na elfu moja na mia tano" amesema.
Amesema kufuatia kauli hiyo waliamua kumpeleka kituo cha polisi kibiti kwa ajili ya kutoa taarifa hiyo na kupewa PF3 kwa ajili ya kupelekwa kufanyiwa uchunguzi katika kituo cha afya Kibiti.
Mganga Mkuu wa kituo cha afya Kibiti Dr Sadock Bandiko amekiri kufikishwa kwa mtoto huyo kituoni hapo na kubainika mtoto huyo alikuwa na uchafu kwenye sehemu zake za siri.
"Ni kweli tu memfanyia uchunguzi na tumemkuta ana uchafu katika sehemu zake za siri japo hatuwezi kuthibitisha moja kwa moja kama uchafu huo ni wa mtuhumiwa au la," amesema Dk Bandiko.

 
Top