BAADA ya Simba, kukosa ubingwa ndani ya miaka mitatu kwa madai kuwa wanatengeza timu, straika wao wa zamani Ulimboka Mwakingwe, amewaambia viongozi wa klabu hiyo kuwa lazima wajenge urafiki na wachezaji wao na kuwafundisha jinsi ya kuishi na si kuwafanya waishi kama wapo jeshini.

Akifafanua kauli hiyo Mwakingwe alisema: “Viongozi Simba wanapenda kuogopwa jambo linalowafanya washindwe kudumu na wachezaji ambao ndiyo wangeunda kikosi makini na tishio kwenye VPL. Wakiishi vizuri na wachezaji wao basi wanaweza kufanya makubwa zaidi ya hayo,”

Mwakingwe alisema Simba ni timu pekee zenye wachezaji vijana ukilinganisha na Yanga na Azam ambazo vikosi vyao vimesheheni wachezaji ambao vipaji vyao vinaelekea ukingoni na kuwataka Simba kuwapa fursa ya kutosha vijana kwa kuwatunza vizuri.

“Hakuna sababu ya kila siku Simba kuwe na stori ya kutimua wachezaji, wabadilike soka la sasa lazima mchezaji ajitambue na asimamie haki zake na si kuogopa kiongozi kwa mtindo huo ni vigumu kufikia malengo.

“Nimecheza kwa mafanikio makubwa si kwamba nilikuwa napitia raha wakati wote, kuna mengi nilikuwa navumilia. Viongozi kutaka kuogopwa kila wakati si sahihi,” alisema.


 
Top