MTOTO mwenye ulemavu wa ngozi (albino) mwenye umri wa miaka mitatu,
mkazi wa wilaya ya Itilima, mkoani Simiyu hivi karibuni amenusurika
kuuawa kwa kukatwa mapanga, baada ya bibi yake kudaiwa kumuuza kwa
wauaji hao ili waweze kuchukua sehemu ya viungo vyake.
Mtoto huyo alinusurika kifo baada ya wauaji hao kufika nyumbani kwao
majira ya jioni na kumkuta akiwa na mama yake mzazi na ndipo wakamkwapua
na kutaka kukimbia naye, lakini mama yake akafanikiwa kumuokoa baada ya
kupambana na kunyang’anyana hadi kusababisha mtoto huyo kuchubuka mkono
mmoja.
Hayo yalielezwa juzi na Mkurugenzi wa Kituo cha Kulelea Watoto wa
makundi Maalumu cha Bikira Maria Mama wa Mungu Msaada Daima, Sista Maria
Hellena, kwenye maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika
juzi katika kata ya Lamadi, wilayani hapa.
“Hao wauaji walifika nyumbani kwao na mtoto huyo na kumkuta akiwa na
mama yake mzazi, sasa wakamkwapua na kuanza kunyang’anyana, mama mtoto
alifanikiwa kumuokoa mikononi mwa watu hao, lakini ngozi ya mkono
ilichubuka sana ndipo wakamleta hapa na tunaendelea kumlea hapa
kituoni,” alisema Sista Hellena.
Aidha, Sista Hellena alisema bibi wa mtoto huyo na wauaji hao walitoroka na kesi iko Polisi.
Katika hatua nyingine, Sista Hellena alisema kuwa watoto wengi
wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili na wazazi wao, na kusema kama
wanashindwa kuwalea baada ya kuwazaa ni bora wawapeleke kwenye kituo
chake, hata kwa kuwatelekeza nje ya kituo hicho ili aweze kuwachukua.
Mratibu wa Kituo hicho, Belensi China, alisema watoto wanakabiliwa na
changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kupewa kazi ngumu ya kuchunga
mifugo.